Miili ya maaskari ikishushwa kwa ajili ya taratibu za mazishi.Picha ya Maktaba. 
Ni majonzi yasiyosahaulika katika kumbukumbu za Kitaifa nchini kufuatia mauaji ya wanajeshi tisa wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JTWZ);  waliuawa wakiwa katika harakati za kulinda amani huko Darfur Sudan Kusini pamoja na mapigano ya kuwaondoa waasi wa M23 nchini DRC Kongo.
Itakumbukwa Tanzania ilishiriki katika kuondoa machafuko katika nchi mbalimbali hasa DRC Kongo, Sudan na Sudan Kusini kutokana na azimio la Umoja wa mataifa la kulinda amani katika mataifa yenye machafuko ya amani namba 6&7.
Kutokana na azimio hilo Tanzania ikaungana na kikosi cha Umoja wa mataifa cha kulinda amani jimbo la Darfur baada ya kupeleka askari wake 850 kwa lengo la kuongeza nguvu ya kumaliza mapigano hayo.
Kwa upande wa DRC Kongo, Majeshi ya Tanzania yalipelekwa kulinda amani chini ya Umoja wa Mataifa pia huku wakiungana na nchi za Afrika Kusini na Malawi kukamilisha kikosi cha wanajeshi 3,000 waliokuwa tayari kutuliza mapigano hayo. 
Waliouawa Darfur
Tukio la kwanza lilitokea Julai,12  mwaka jana baada ya kuripotiwa kuuawa kwa askari saba wa JWTZ ambao walikuwa miongoni mwa kikosi cha Umoja wa Mataifa cha kulinda amani katika jimbo la Darfur nchini Sudan.
Wanajeshi hao walifariki kutokana na mashambulizi yaliyofanywa na waasi wanaopigana na Serikali.
Tukio hilo kwa mara ya kwanza liliripotiwa kuwa mojawapo ya tukio kubwa kuwahi kutokea kwa askari wa Tanzania kuuawa kwa wakati mmoja ukilinganisha na Agosti mwaka 2012  ambapo wanajeshi watatu wa Tanzania waliouawa huko Darfur katika tukio kama hilo.
Aliyekuwa Msemaji wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), Kanali Kapambala Mgawe alisema wanajeshi hao walikuwa wametawanywa kwenye miji ya Khor Abeche na Muhajeria kusini mwa Darfur.
Wachambuzi na Wanadiplomasia mbalimbali duniani wanasema machafuko ya Darfur hayatamalizika mpaka Serikali itakapotafuta suluhisho la matatizo ya kudumaa kwa maendeleo, kutengwa kisiasa na kupotea kwa rasilimali.
Kutokana na machafuko hayo, mpaka sasa Rais wa Sudan, Omar Hassan Al Bashir, ameshtakiwa na Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu, ICC, kwa makosa ya mauaji ya kimbari, uhalifu wa kivita na uhalifu dhidi ya binadamu makosa yaliyotekelezwa Darfur.
Wakati majeshi ya Tanzania yakiendelea kuwa nchini humo, mapigano hayo yameendelea kuripotiwa kushika kasi magharibi mwa Sudani katika jimbo hilo la Darfur.Kumbukumbu ya Darfur
Mzozo wa Darfur ulianza miaka 10 iliyopita baada ya waasi kuanza kushambulia maeneo ya Serikali, wakiishutumu Khartoum kwa kuwakandamiza watu wenye asili ya Afrika na kuipendelea jamii ya Kiarabu.
Kundi la wanamgambo wa Kiarabu la Janjaweed, wakati huo lilishutumiwa kwa kuendesha mauaji ya kikabila dhidi ya raia Waafrika wa Darfur.
Mbali na amani kuanza kurejea katika eneo hilo, Umoja wa Mataifa, umeripoti zaidi ya watu 300,000 wamepoteza maisha kutokana na mzozo huo wa Darfur huku Serikali ya Khartoum imekuwa ikiripoti idadi yao ni 12,000 tu.
Kwa mujibu wa taarifa ya Shirika la Utangazaji la BBC, tangu kuanza kwa machafuko hayo, kuna watu wengine zaidi ya milioni 1.4 walioachwa bila makazi.
Chanzo cha  kutokea kwa machafuko ya Darfur mwezi februari mwaka 2003,yalianza wakati Jeshi la Ukombozi la Sudan likiwa na harakati ya haki na usawa ambapo liliamua kuchukua silaha na kuanza kushutumu Serikali kwa kuwadhulumu Waafrika huku ikiwapendelea Waarabu.