“Nitasha- ngaa sana iwapo wajumbe wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar wataupinga mfumo wa Serikali Tatu...”Ali Saleh.PICHA MAKTABA 
Zanzibar.
 Kamishna wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Ali Saleh amesema atawashangaa wajumbe wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar (BLW), iwapo watapinga mfumo wa Serikali tatu uliopendekezwa katika Rasimu ya Pili ya Katiba.
Akizungumza mwishoni mwa wiki kwenye semina maalumu ya kujadili rasimu ya pili ya Katiba iliyofanyika kwenye Ukumbi wa Taasisi ya Kiswahili na Lugha za Kigeni na kuhudhuriwa na makamishna sita wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Zanzibar, alisema mfumo wa Serikali mbili unaotetewa na CCM umeshindwa kutatua kero za Muungano kwa miaka 50 iliyopita na hakuna njia mbadala zaidi ya kujiondoa katika mfumo.
“Nitashangaa sana iwapo wajumbe wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar wataupinga mfumo wa Serikali Tatu, kwa kuwa muda mrefu wamekuwa wakizungumza jambo hilo hata kulipendekeza kama ufumbuzi wa kudumu,” alisema Saleh ambaye kitaaluma ni mwanasheria.
Alisema mambo yasiyokuwamo katika orodha ya mambo ya Muungano yamekuwa na wakati mgumu kwa miaka 50 na Zanzibar kushindwa kunufaika moja kwa moja, huku upande wa pili wa Muungano ukinufaika nayo.
Hata hivyo, Mwakilishi wa Viti Maalumu na Makamu Mwenyekiti wa UWT Zanzibar, Asha Bakari Makame alisema hakubaliani na madai ya Saleh kuwa mapendekezo ya wawakilishi ni mfumo unaopendekeza Serikali tatu.
Asha alisema hakumbuki iwapo wawakilishi waliwahi kutoa pendekezo la pamoja na kuunga mkono Serikali tatu na kuwa haipaswi kutiliwa maanani.
“Sikubaliani na dai la Kamishna Saleh…Naomba afute usemi wake na kutuomba radhi,” alisema Bakari.
Alisema hakukuwa na haja ya kuendelea kufanyika makongamano, warsha wala semina kwa kuwa kazi ya Tume ya Mabadiliko imegota ukingoni baada ya kukusanya maoni ya wananchi na kuandika Rasimu ya pili ya Katiba.