Muhongo alisema kuwa katika awamu ya kwanza ya miradi iliyomalizika Desemba mwaka jana, wanavijiji walilipa gharama kubwa, hivyo Serikali imeamua kupunguza malipo hayo, ili huduma hiyo ya nishati iwafikie watu wengi zaidi.PICHA|MAKTABA
Dar es Salaam. Serikali imetangaza kupunguza gharama za kuunganisha umeme kutoka Sh177,000 za awali hadi Sh27,000 vijijini.
Awali, punguzo hilo lilitolewa kwa mikoa ya Lindi na Mtwara, ambako bomba la kusafirisha gesi kwenda Dar es Salaam limeanzia, lakini sasa gharama hizo zitakuwa kwa vijiji vyote nchi nzima.
Akizungumza jijini Dar es Salaam jana, Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo alisema gharama hizo zitahusu miradi inayosimamiwa na Wakala wa Umeme Vijijini (REA) katika kipindi ambacho makandarasi watakuwa wakiendelea na awamu ya pili ya miradi inayotarajiwa kuanza Machi mwaka huu.
Muhongo alisema kuwa katika awamu ya kwanza ya miradi iliyomalizika Desemba mwaka jana, wanavijiji walilipa gharama kubwa, hivyo Serikali imeamua kupunguza malipo hayo, ili huduma hiyo ya nishati iwafikie watu wengi zaidi.
Hata hivyo, ofa hiyo itadumu kwa mwaka mmoja na miezi mitano pekee, kwani awamu ya pili ya miradi hiyo inatarajiwa kuanza Machi, 2014 na kumalizika Juni, 2015.
“Gharama hizo ni kwa kipindi ambacho makandarasi watakuwa kazini tu. Makandarasi msiwakatalie wanavijiji kuwafungia umeme,” alisema Muhongo.
Waziri Muhongo aliwanyooshea kidole makandarasi wa miradi ya umeme vijijini akisema kuwa wanalalamikiwa kwa kuomba rushwa kwa wanavijiji ili wawaunganishie umeme kwenye nyumba zao.
“Kule Bunda kuna mwanakijiji alimtaja mfanyakazi wa kampuni inayoomba rushwa… kampuni hiyo imeshapewa onyo, ninapendekeza isipewe tena kazi,” alisema Muhongo.
Pia alilitaka Shirika la Ugavi wa Umeme nchini (Tanesco) na REA kutokutumia gharama kubwa kulipa fidia za majengo au mashamba ya wanavijiji kwa kuwa historia inaonyesha kuwa zoezi hilo huambatana na rushwa.
“Tuna historia mbaya linapokuja suala la fidia, limejaa rushwa tupu,” alisema.