Simu za mkononi ambazo zimekuwa zikitumika kurahishisha mawasiliano. Simu hizi zimepigwa marufuku na vyombo vya sheria kutumika miongoni mwa wafungwa wanaotumika adhabu zao. Picha na AFP.
Nairobi.
Zaidi ya simu 600 za mkononi pamoja na takriban laini 5,000 za simu zimenaswa katika gereza la Kamiti Maximum baada ya msako wa kushtukiza uliofanywa chini ya usimamizi mkuu wa gereza hilo.
Naibu ofisa mkuu katika gereza hilo, Patrick Isaboke alisema msako huo uliodumu kwa siku nne ulifanywa baada ya uchunguzi kubaini kuwepo na ujumbe mwingi wa kutishia raia hutoka magerezani. Isaboke alisema kuwa hawakuweza kuwajua wafungwa wanaomiliki simu hizo kwani walitolewa wote ndani ya sehemu wanazoishi ndani ya gereza hilo, kabla ya msako kufanywa.
Msako huo umethibitisha hofu kwamba Gereza la Kamiti linahusika kwa kiasi kikubwa katika visa vya utekaji nyara jijini Nairobi na viungani mwake, kutokana na mawasiliano ambayo yamekuwa yakiendelea baina ya wafungwa waliopo gerezani humo na jamaa au makundii yao yaliyopo uraiani.
Juzi, wafungwa walizua vurugu baada ya msako. Katika vurugu hizo, wale walioitwa kuripoti katika viwanda vya gereza hilo waligoma na badala yake kuandamana. Walinzi walilazimika kufyatua risasi hewani ili kutuliza vurugu hizo.
Angalau wafungwa wanne walijeruhiwa lakini wasimamizi wa gereza hilo walikataa kutoa taarifa yoyote kuhusu kisa hicho, kwa kuwa taarifa za mambo mengi yanayoendelea ndani ya magereza hufanywa siri.
Taarifa zilieleza kwamba baadhi ya walinzi walizidiwa wakati wa vurugu hizo na ikamlazimu mkuu wa gereza hilo kuwaita walinzi kutoka magereza mengine na wale walio katika Chuo cha Magereza cha Ruiru.
Vyanzo muhimu katika tukio hilo vilikaririwa vikieleza kwamba ofisa mkuu wa Serikali alimwamuru Waziri wa Usalama, Joseph ole Lenku kufanya msako wa kunasa vitu visivyoruhusiwa magerezani baada ya uchunguzi kuhusu kisa cha utekaji nyara kuonyesha kuwa kilikuwa kinapangwa gerezani humo.
Ingawa maofisa hao wanapaswa kuwafanyia msako wafungwa wote, ripoti zinaeleza kuwa baadhi ya walinzi wa gereza wanashirikiana na wafungwa ili kupeleka vitu hivyo haramu gerezani. Duru zinasema kuwa maofisa hao huwauzia wafungwa simu hizo.
“Baadhi ya wafungwa hawaadhibiwi wanapokutwa wakiwa wanamiliki vitu haramu kama hivyo, ambavyo kimsingi huwa havitakiwi kabisa kuwepo gerezani. Kuna viranja ambao ni macho ya walinzi katika kila seli,” alisema mlinzi mmoja wa cheo cha chini ambaye aliomba asitajwe jina.
Ilielezwa kwamba mara nyingi simu hubebwa na maofisa wakuu ambao huwa hawafanyiwi msako wanapoingia katika taasisi hiyo. Maofisa hao hukabidhi simu hizo kwa walinzi wanaosimamia vitengo tofauti.
|
0 Comments