Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe akizungumza kwenye mkutano na waandishi wa habari, Dar es Salaam jana. Picha na Fidelis Felix 

Dar es Salaam.
 Serikali inatarajia kupeleka kikosi kimoja cha Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) huko Sudan Kusini kwa ajili ya kulinda amani kutokana na vita ya wenyewe kwa wenyewe inayoendelea.
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe alisema Dar es Salaam jana kwamba Serikali imekubali kupeleka batalioni moja baada ya kuombwa na Umoja wa Mataifa (UN).
Sudan ya Kusini imekuwa katika machafuko ambayo yamesababisha vifo vya mamia ya raia na wengine kujeruhiwa.
 “Tumefanya uamuzi wa kupeleka majeshi yetu Sudan Kusini, tumefanya hivyo baada ya kuombwa na Umoja wa Mataifa kwa sababu ya ubora wa jeshi letu,” Membe aliwaambia waandishi wa habari.
Alisema jukumu la kulinda amani katika Bara la Afrika ni la Waafrika wenyewe na kwamba Tanzania inajiona kwamba ina jukumu la kusaidia kupatikana kwa amani.
Alisema Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-Moon alimwomba Rais Jakaya Kikwete kusaidia kupeleka majeshi yake Sudan Kusini kusaidia kulinda amani. “Rais alikubali, sasa tuko kwenye maandalizi, nadhani Aprili jeshi letu litaondoka kuelekea Sudan Kusini,” alisema Membe.
Kwa sasa Tanzania ina vikosi vya wanajeshi wa kulinda amani katika nchi za DRC, Darfur(Sudan) na Lebanon.
Mgogoro Ziwa Nyasa
Kuhusu mgogoro wa mpaka kati ya Tanzania na Malawi katika Ziwa Nyasa, Membe alisema utapatiwa ufumbuzi mwezi ujao baada ya mawaziri na maofisa wa nchi hizo kuwekwa kitimoto na Kamati ya Rais Joaquim Chisano wa Msumbiji na viongozi wengine wastaafu.
Membe alisema wanaotakiwa kwenda kuhojiwa ni yeye na maofisa wake na Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Profesa Anna Tibaijuka na Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Jaji FrederickWerema… “Baada ya pande mbili za viongozi kutoka Tanzania na Malawi kuwekwa kitimoto, ndipo uamuzi utatolewa.”
Alisema anaamini kwamba uamuzi huo utakuwa mpaka kuwa katikati ya Ziwa Nyasa, badala ya ziwa lotekuwa mali ya Malawi.
Alisema kama uamuzi utakuwa ziwa lote kuwa mali ya Malawi, Tanzania itawasilisha mashtaka katika Mahakama ya Kimataifa ya Usuluhishi wa Migogoro (ICJ).Membe alisema kabla ya uamuzi huo, maofisa kutoka Tanzania na Malawi wameshahojiwamara tatu katika mikutano iliyofanyika Maputo, Namibia na Dar es Salaam.
Tanzania kuteketeza meno ya ndovu
Akizungumzia biashara haramu ya meno za ndovu, Waziri Membe alisema kuna uwezekano wa Tanzania kuteketeza shehena ambayo imehifadhiwa nchini baada ya kushinikizwa na taasisi mbalimbali za kimataifa.
Alisema lengo la Tanzania lilikuwa kuuza nyara zilizokamatwa, yakiwamo maelfu ya tani za meno hayo ili kupata fedha za kununulia vifaa vya ulinzi wa wanyama kwenye hifadhi za taifa, lakini haikufanikiwa.
Uamuzi wa kuziteketeza au la utatolewa na Waziri wa Maliasili na Utalii atakaporejea kutoka Uingereza, kutokana na kushinikizwa na Shirika la Kimataifa la kulinda wanyama walio hatarini kutoweka (Cites).
Uraia wa nchi mbili
Membe alisema wizara yake itaendelea kueleza umuhimu wa wananchi kuwa na uraia wa nchi mbili ili kuwasaidia Watanzania wanaoishi nje kuleta maendeleo nyumbani.
Alisema sheria iliyopo sasa inaruhusu raia wa nje akiishi Tanzania kwa miaka 10, kukubaliwa kuwa raia akiomba lakini Mtanzania akiishi nje ya nchi akapata uraia anafutiwa uraia wa nyumbani.
Sheria hii inaonyesha kuwathamini wageni kuliko Watanzania ambao wakiukubali uraia wa nchi nyingine wanafutiwa wa Tanzania.
“Tunataka sasa uraia wa nchi mbili na kwa kuwa suala hilo limo kwenye Rasimu ya Katiba, tutawaelimisha wananchi waweze kufahamu faida za uraia wa nchi mbili,” alisema Membe.
Tanzania na Rwanda
Kuhusu uhusiano wa Tanzania na Rwanda, Membe alisema kumekuwa na vita ya maneno inayotolewa na vyombo vya habari vya nchi hiyo jirani.Alisema Rwanda ikumbuke kuwa Tanzania imekuwa kituo cha wapigania uhuru tangu 1963 na kwamba vyama vya wapigania uhuru viliweka kambi nchini kwa sababu walifahamu kwamba Tanzania inataka nchi zote za Bara la Afrika kujikomboa na kuwa na amani.
Alisema vita ya maneno inayofanywa na vyombo vya habari vya Rwanda ni dalili za kuonyesha kutokuiamini Tanzania lakini wafahamu kwamba nchi hii bado inalinda misingi ya amani.