Ndege iliyotekwa ikiwa imetua nchini Uswisi. Picha ya Maktaba 
Msaidizi wa rubani wa ndege ya Shirika la Ndege la Ethiopia, Halimedhin Abera, ndiye aliyebainika kuteka moja ya ndege za shirika hilo hivi karibuni.
Inadaiwa kuwa rubani huyo aliiteka ndege kwa sababu ya kuwa na msongo wa mawazo, baada ya kufiwa na mjomba wake.
Abiria mmoja aliyenusurika katika ajali hiyo anasema, Abera aliwaamuru abiria wote kukaa chini, huku akiwatishia kuzima hewa  ya Oksijeni.
Abera, ambaye amelifanyia kazi shirika hilo kwa miaka mitano, inadaiwa  alifunga mlango wa chumba cha rubani (cockpit) na kubadilisha mwelekeo wa ndege. Awali ndege hiyo ilikuwa ikielekea Italia, lakini akaamua kuipeleka Uswisi aliposema alikwenda kuomba hifadhi. Msimuliaji huyu wa mkasa  anasema baada  ya kuiteka ndege alifungua maski za hewa ya oksijeni na kutishia kuizima kama abiria wasingetulia.
Anasimulia: “Nilifikiri labda kuna tatizo la kiufundi au kwa bahati mbaya mtu amebonyeza sehemu, abiria tulibaki  tukitazamana kwa sura za kuulizana ndani ya ndege.”
Anasema baada  ya muda mfupi, sauti nzito ikizungumza kwa jazba ilisikika kutoka katika vipaza sauti vya ndege ikisema: “Kaa chini, ninazima hewa ya oksijeni”.
Msimuliaji anasema rubani huyo alikaa kimya kwa saa sita bila kuzungumza, huku abiria wakiwa hawajui wanaelekea wapi wala mwisho wao utakuwa vipi.
Anaongeza kusema kuwa  wakati hayo yanaendelea, wahudumu wa ndege waliendelea kugawa vinywaji, huku wakiwatuliza abiria na kuwahakikishia kuwa safari ilikuwa salama.
Hata hivyo, wahudumu hao waliwaambia kuwa, hawana mawasiliano na rubani huyo kwa kuwa ameyakata.
“Wahudumu walikuwa wanagawa vinywaji na kutoa maneno ya faraja, hata hivyo kuna wengine walikuwa wakitokwa machozi mbele yetu,” anasema msimuliaji.
Baada ya kusafiri saa sita kimyakimya, ghafla ndege ilianza kuzunguka huku ikiegemea upande mmoja na baada ya muda ilibadilisha upande wa bawa jingine.
Anasema: “Niliona mwisho wetu umefika kwani ndege sasa inaanguka. Nikitazama nje niliona mwanga lakini baada ya dakika mbili nikaona giza tena,” anasema na kuongeza:“Ndege ikaanza kwenda kasi, naiona ndege ikipita juu ya nyumba. Nilipotazama tena chini nikaouona uwanja wa ndege,” anasema.
Anasema iliposimama ndipo waliambiwa habari za rubani huyo kuiteka ndege, kwani muda wote walikuwa hawafahamu kilichokuwa kikiendelea.
Mjomba wa Abera, Alemu Asmamaw ameliambia shirika la habari la Associate Presskuwa kitendo hicho anakihusisha na msongo wa mawazo, kwani hivi karibuni alipata msiba wa mjomba wake mwingine.
Ndege hiyo ilifanikiwa kutua salama kwa msaada wa ndege za kivita za Ufaransa, pia baada ya kumkubalia rubani huyo ombi lake la kutaka hifadhi nchini humo.
Matukio mengine ya utekaji Ethiopia
Mwanamume mmoja mwenye asili ya Ethiopia mwaka 1993 aliiteka ndege ya  Shirika laLufthansa na kuiamrisha impeleke Marekani kwa kuwa alikataliwa viza ya kuingia nchini humo.
Juni, 1994, Ndege ya Shirika la Ethiopia ilitekwa na watu kadhaa ambao walitaka iwapeleke barani Ulaya.
Mwaka  1995, mwanamume mwingine wa Ethiopia alitaka kuiteka ndege kwa kutumia kisu cha wahudumu, akitaka arudishwe Ulaya kwani alikuwa akirudishwa kwao kutokana na matukio mbalimbali ya uhalifu aliyofanya nchini Ugiriki.
Mwaka jana watu watano waliiteka ndege ya Ethiopia wakitaka wapelekwe Ugiriki na Sweden, hata hivyo iligeuzwa na kupelekwa katika Mji wa Al Obeid karibu na mji mkuu wa Sudan, Khartoum.
Ndege kutoka Ethiopia kwenda Ivory Coast ikipitia Kenya ilitekwa na watu  watatu mwaka 1996 wakitaka wapelekwe Australia. Ndege hiyo iliishiwa mafuta na kuanguka katika Visiwa vya Comoro na kuua watu 125.
Katika tukio jingine, marubani watano wa jeshi  waliokuwa katika majaribio katika Mji wa Bahr Dar, Ethiopia walilazimisha wapelekwe Saudi Arabia.
Makala haya yameandikwa kwa msaada wa mtandao.