“Madaraka ya Bunge Maalumu yanakuwa na mipaka endapo Rasimu ya Katiba imeandaliwa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba au chombo cha aina hiyo.PICHA|MAKTABA 

Dar es Salaam
Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Warioba amesema litakuwa jambo lisilo la kawaida kwa Bunge Maalumu la Katiba kubadili hoja ya msingi iliyopo kwenye Rasimu ya Katiba, akisisitiza kuwa jukumu lake ni kuifanyia marekebisho.
Akihutubia mkutano ulioandaliwa na Kituo cha Demokrasia Tanzania (TCD), wa tafakuri na maridhiano kuelekea Katiba Mpya jana, Jaji Warioba alisema:
“Madaraka ya Bunge Maalumu yamekuwa yanabadilika kwa kutegemea aina ya mchakato unaotumika. Afrika Kusini, Namibia na Cambodia, Bunge Maalumu lenyewe ndilo lilipewa jukumu la kuandika Rasimu ya Katiba. Katika mazingira haya, Bunge Maalumu lilikuwa na madaraka ya kubadilisha mambo mengi katika Rasimu ya Katiba… lilikuwa na madaraka ya kuachana na Rasimu ya Katiba na kuandika Rasimu Mbadala.
“Madaraka ya Bunge Maalumu yanakuwa na mipaka endapo Rasimu ya Katiba imeandaliwa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba au chombo cha aina hiyo.
Bunge Maalumu linaweza kuwa huru kurekebisha baadhi ya masharti yaliyomo kwenye Rasimu ya Katiba lakini si suala la kawaida Bunge Maalumu kubadili hoja ya msingi. Jinsi ushirikishaji wa wananchi unavyokuwa wa wazi na mpana ndivyo madaraka ya Bunge Maalumu yanavyopungua.”
“Mantiki ni kuzuia Bunge Maalumu kunyang’anya madaraka ya wananchi, yaani “act of popular sovereignty”. Wataalamu wa masuala ya Katiba wanaeleza kuwa madaraka ya Bunge Maalumu katika mazingira haya ni kuboresha Rasimu ya Katiba.
“Kwa mujibu wa Kifungu cha 25(1) cha Sheria ya Mabadiliko ya Katiba, Sura ya 83, Bunge Maalumu limepewa madaraka ya kujadili na kupitisha masharti ya Katiba, kutunga Sheria ya Masharti ya Mpito na Masharti yatokanayo na kabla ya kuanza kazi hiyo, Bunge Maalumu litapitisha Kanuni za Bunge Maalumu ambazo zitaongoza utekelezaji wa mamlaka ya Bunge Maalumu.”
Bunge Maalumu la Katiba litaanza kukutana Jumanne ijayo kujadili Rasimu ya Katiba iliyotolewa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba Desemba 30, mwaka jana.
Moja ya masuala yanayotazamiwa kusababisha mvutano mkubwa kwenye vikao vyake ni lile la muundo Muungano na hasa suala la Serikali Tatu uliopendekezwa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba.
Chama Cha Mapinduzi (CCM) kinataka kusukuma ajenda ya kuendelea kwa muundo wa Serikali Mbili Bunge la Katiba wakati vyama vya upinzani vinataka mapendekezo ya Tume ya Mabadiliko ya Katiba ya Serikali tatu yaheshimiwe.
Jaji Warioba alisema Bunge Maalumu linapaswa lifanye kazi ya kuboresha masharti ya kikatiba yaliyomo ndani ya Rasimu ya Katiba pasipo kuweka masharti mapya ambayo kwa taathira yake yanabadilisha au kufifisha yaliyomo kwenye rasimu hiyo.
Kuhusu mchakato wa kupata Katiba Mpya Tanzania, Jaji Warioba alisema kila mtu anafahamu kuwa ulifuata utaratibu wa kuandaliwa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba ndiyo maana hata Bunge Maalumu la Katiba litakapokutana Dodoma litatakiwa kufuata utaratibu huo.Jaji Warioba alisema utungaji wa Katiba unatakiwa kuwa shirikishi kwa maana ya kuwahusisha wananchi katika hatua zote za mchakato kwa maelezo kuwa kwa kadri mchakato wa kuandika Katiba unavyowashirikisha kwa mapana, ndivyo utakavyoongeza uwezekano wa kukubalika, kuheshimika na utekelezaji wa Katiba utakavyokuwa rahisi.
“Wananchi wanaposhiriki katika utungaji wa Katiba na pale matakwa yao yanapozingatiwa ndani ya Katiba, wananchi hao huimiliki Katiba hiyo na kuiona kuwa ni yao. Wananchi huona hivyo kwa sababu licha ya kushiriki lakini pia Katiba hiyo huakisi utashi wao na ndoto zao na hivyo kukubali kuongozwa na masharti yaliyomo ndani ya Katiba,” alisema.
Apinga kura kupitisha maoni
Akizungumzia upigaji wa kura katika kufanikisha mchakato wa kupatikana kwa Katiba Mpya, Jaji Warioba alionya akisema hatua hiyo itasababisha kuzaa Katiba itakayopingwa na wananchi wengi.
“Bunge la Katiba lina jukumu la kusimamia mchakato mzima wa upatikanaji wa Katiba ya wananchi wote. Kama tunataka kuunganisha Taifa, tukubaliane kwa maridhiano, mkikubaliana kwa kupiga kura siku hiyohiyo Katiba itaanza kupingwa,” alisema Jaji Warioba.
Dk Bilal asema kura itaamua
Akifungua mkutano huo, Makamu wa Rais, Dk Mohamed Gharib Bilal alisema suala la mchakato wa Katiba ni zito na hutokea mara chache katika maisha hivyo kumtaka kila aliyepata wasaa wa kushiriki katika Bunge Maalumu la Katiba, kutumia fursa kwa busara.
Dk Bilal alisema ni vizuri wanasiasa na wadau wote kujiandaa kupokea matokeo ya kura kama itakavyopigwa na wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba.
Aliwataka viongozi wa vyama vya siasa kuonyesha mfano kwa kuhubiri amani ili mchakato wa Katiba umalizike kwa amani huku kila mmoja akiweka masilahi ya taifa kwanza na yale ya kisiasa baadaye.
“Katiba ni yetu wote, hatuna haja ya kutoana ngeu… tukiweka Tanzania kwanza tutafanikiwa, lakini tukiweka masilahi yetu ya siasa mbele hatuwezi kufanikiwa… kila mmoja wetu atumie fursa hii kwa busara,” alisema.
Mbatia atoa angalizo
Mwenyekiti wa TCD, James Mbatia alisema Katiba siyo mali ya viongozi na wanasiasa, bali ni ya wananchi wote na kuwakumbusha wote waliopewa jukumu la kuiandaa kuelewa kuwa wananchi wanataka Katiba inayoakisi ndoto na matarajio yao na itakayopunguza na au kuondoa hofu waliyonayo ya kuzidi kuwa maskini na fukara.“Katiba haipatikani kwa wingi wa kura, balikwa kugusa mioyo ya kila anayeshiriki kuona kwamba amekuwa sehemu ya maridhiano yaliyopatikana. Ni vizuri tukubaliane leo na kesho kuweka misingi ya pamoja ya kuhakikisha tunapata Katiba Mpya kwa njia ya kujadiliana na kuridhiana,” alisema Mbatia, ambaye pia ni Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi.