Add captiokatuni ikionyesha mama akimnywesha pombe ya kienyeji mtoto wake, imeelezwa kuwa wazazi wengi hupenda kuwapatia pombe watoto wao ili wapate usingizi ili waweze kufanya kazi zao zingine.
Dar/Iringa.
 Inawezekana kuwa baadhi ya wazazi mkoani Iringa, wanamuunga mkono kwa vitendo mwanafalsafa na mwandishi maarufu wa Marekani, Benjamin Franklin, aliyewahi kusema: “Katika mvinyo kuna hekima, ndani ya bia mna uhuru na ndani ya maji kuna bakteria.”
Ingawa kauli ya Franklin iliishia katika maneno, baadhi ya wazazi wakulima katika vijiji mbalimbali mkoani Iringa, wanautekeleza usemi huo kwa vitendo kwa kuwanywesha pombe za kienyeji watoto wao wadogo wanapokuwa shambani, ili walale usingizi ili wazazi hao wapate nafasi ya kulima bila usumbufu.
Uchunguzi uliofanywa na gazeti hili na kuzungumza na baadhi ya wazazi katika maeneo hayo, umebaini kuwa utamaduni huo umekuwapo kwa miaka mingi mkoani humo.
Baadhi ya wazazi waliozungumza na gazeti hili wanasema kuwa ingawa bado wapo baadhi ya watu wanaoendelea na vitendo hivyo, lakini ukweli ni kwamba tayari vijana wengi wameshapata madhara yatokanayo na pombe hiyo ya utotoni.
Wanaofanya kitendo hicho wanasema kuwa wanapofika shambani kwanza huwatafutia watoto wao eneo zuri la kivuli na kuwatandikia vyema, kabla ya kuwanywesha pombe, kisha ndipo mzazi huanza kulima.
Lameck Kihaga, mkulima katika eneo la Itagutwa, anaeleza kuwa zamani ilikuwa kawaida kwa mzazi kumnywesha mtoto wake kikombe kimoja au viwili vya pombe kama dawa ya usingizi.
Anasema kwamba tabia hiyo imesababisha ongezeko kubwa la wanywaji pombe maarufu aina ya ulanzi au komoni mkoani humo ambao bado ni vijana wadogo na wanafunzi wa shule za msingi na sekondari.
“Naamini kabisa, hawa vijana walevi mitaani leo, wengi wao wamelowea kutokana na tabia ya kunyweshwa pombe wakiwa bado wadogo,” anasema Kihaga.
Kauli ya Serikali
Ofisa Maendeleo ya Jamii, Mkoa wa Iringa, Menrad Dimoso anasema kuwa taarifa za wazazi kuwanywesha watoto wao pombe za kienyeji wakati wa kilimo zimekuwapo muda mrefu mkoani humo, lakini siyo tatizo kubwa.
Anasema kwamba wazazi wengi waliokuwa wakifanya vitendo hivyo walishaacha na wanaoendeleza tabia hiyo ni wachache, hivyo haiwezi kuwa na madhara makubwa kwa jamii.
Kadhalika ziko taarifa kuwa kuwanywesha watoto wadogo pombe huweza kuwasababishia wapate utapiamlo na alipoulizwa Dimoso alisema:“Ni kweli nalijua jambo hilo, pombe inaweza kuwafanya wakapata utapiamlo, lakini mtu wa lishe angeweza kukupatia ufafanuzi zaidi.”
Mganga Mkuu wa Hospitali ya Mkoa wa Iringa, Dk Ezekiel Mpuya, anasema kuwa pombe hizo za kienyeji zina madhara sawa na pombe nyingine zozote. Anataja madhara hayo kuwa ni pamoja na kuathiri ukuaji wa mtoto kiakili na maendeleo yake ya kiafya.
“Jambo hili lilikuwa kubwa sana zamani, sijalisikia katika siku za hivi karibuni,” anasema Dk Mpuya.
Daktari Bingwa wa Watoto katika Hospitali ya Amana, Dar es Salaam, Dk Mtagi Kibatala anasema unywaji pombe kwa watoto wadogo una madhara makubwa kiafya ikiwa ni pamoja na kupata matatizo ya ubongo.
Anaeleza kuwa kitendo cha mzazi kumlazimisha mtoto wake mdogo alale usingizi kwa pombe, kinapaswa kupigwa vita kwa kuwa kinaulazimisha ubongo wa mtoto kulala muda mrefu zaidi.
“Nimeshtushwa sana na taarifa hizo, kwa sababu ubongo wa watoto hao hauwezi kuwa sawa, pia wanaweza kupata matatizo kwenyeini,” anasema Dk Kibatala.
Mkazi wa Nduli mkoani Iringa, Grace Kilave anakwenda mbali zaidi na kusema kuwa watoto wengine hunyweshwa pombe wakiwa na umri wa kati ya miaka mitatu hadi mitano, jambo linalowafanya kuizoea na kuiilia kila wanapoona kinywaji hicho.
“Kuna watoto wadogo wamezoea ulanzi kiasi kwamba hata hawajui tofauti ya pombe hiyo na juisi,” anasema Kilave na kuongeza;
“Ninamshukuru Mungu, mimi sikupita kwenye njia hiyo, pengine leo ningekuwa mtu tofauti kabisa.”
Kauli ya Mchungaji
Kwa upande wake, Mchungaji wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Usharika wa Mkwawa, Thadei Kihwaga, anaitaja tabia hiyo kuwa ni mpango wa kubomoa nguvu kazi ya baadaye ya taifa.
“Mbali na kupata utapiamlo, mtoto huyo akikua atatumia fedha zake kwa pombe na ngono zembe,” anasema Mchungaji Kihwaga.Mkazi wa Kihesa Sokoni, Iringa Mjini, Chesko Mlelwa anasema kuwa umefika wakati sasa Serikali na Mashirika Yasiyo ya Kiserikali kuanzisha kampeni maalumu kupinga tabia ya kuwapa pombe watoto wadogo.
“Hapa kwetu hiyo tabia imekuwapo kwa siku nyingi sana, siyo tu shambani hata nyumbani kuna wazazi wanawapa pombe watoto wao,” anasema Mlelwa.
Kwa mujibu wa mtandao wa Wikipedia, nchi zinazoongoza kwa unywaji wa pombe duniani ni Moldovia, Jamhuri ya Czech na Hungary, huku Tanzania ikishika nafasi ya 64 katika orodha hiyo.
Kwa upande wa Afrika, Nigeria ndiyo iliyotajwa kuwa na walevi wengi, ikifuatiwa naUganda, Rwanda, Namibia na Afrika Kusini. Katika orodha hiyo, Uganda inaongoza dunia kwa kunywa pombe za kiasili.(mataputapu).