Mshambuliaji wa Yanga, Emmanuel Okwi (katikati) akiwatoka mabeki wa Ruvu Shooting, Stephano Mwasika (kulia) na Shabaan Suzan wakati wa mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara, jana kwenye Uwanja wa Taifa. Yanga ilishinda 7-0. Picha na Michael Matemanga
Mabingwa watetezi Yanga wametuma salama kwa Al Ahly baada ya kuisambaratisha Ruvu Shooting kwa mabao 7-0, huku Mbeya City wakinyukwa 2-0 na Coastal Union.
Yanga inayojiandaa na mechi ya Ligi ya Mabingwa dhidi ya Al Ahly wiki ijayo ilipata mabao yake kupitia washambuliaji wake Didier Kavumbagu, Simon Msuva waliofunga mabao mawili kila moja, huku Emmanuel Okwi, Mrisho Ngassa na Khamisi Kiiza kila moja alifunga bao moja.
Kwa matokeo hayo Yanga imefikisha pointi 39, wakati Mbeya City waliopokea kipigo wamebaki nafasi ya tatu na pointi zao 35, Azam wameshuka nafasi ya pili na pointi 36 na Simba ya nne (32).
Kipigo cha Ruvu Shooting cha mabao 7-0 kimekuja ikiwa ni siku nne tu zimepita tangu ndugu zao wa JKT Ruvu kunyukwa 6-0 na Tanzania Prisons.
Yanga ilianza mechi hiyo kwa kishindo kwa kupata bao katika dakika ya kwanza lililofunga na Kavumbagu kwa shuti la mguu wa kushoto akipokea pasi ya Okwi, wakati Shooting wakishangaa Msuva aliifungia Yanga bao la pili dakika ya pili akimalizia pasi ndefu ya Ngassa.
Shooting waliamka na kufanya shambulizi dakika ya 12, lakini mpira wa kichwa wa Michael Aidan ulidakwa na Deogratus Munishi.
Kocha msaidizi wa Yanga, Boniface Mkwasa aliyekuwa Misri kuishuhudia Al Ahly aliingia uwanjani hapo dakika 15 na kwenda moja kwa moja kwenye benchi.
Mshambuliaji Okwi aliwainua mashabiki dakika ya 28 kwa kupachika bao la tatu baada ya kumlamba chenga kipa wa Shooting, Abdallah Ramadhani.
Ngassa aliendeleza kulizamisha jahazi la Shooting dakika ya 34 baada ya kumzidi ujanja beki Mangasi Mbonosi na kipa wake Ramadhani na kufunga bao la nne.
Kasi ya washambuliaji wa Yanga, Kavumbagu, Okwi, Ngassa na Msuva iliwashinda kabisa mabeki wa Shooting.
Kocha wa Shooting, Tom Olaba aliwapumzisha Juma Nade, Hamis Ali, Shabaan Suzan na kuwaingiza Said Madega, Ayoub Kitala na Gedion Sepo.
Wakati Hans Pluijm aliwapumzisha Mbuyu Twite, Ngassa, Kavumbagu na kuingia Juma Abdul, Kiiza na Said Bahanuzi.Mabadiliko hayo yalikuwa na faida kubwa kwa Yanga, katika dakika ya 53, Kavumbagu alitumia vyema krosi ya Msuva kufunga bao la tano.
Kiiza alipachika bao la sita kwa kuunganisha krosi ya Msuva bao lililomfanya kocha wa Shooting, Olaba kuondoka uwanjani hapo na kuingia vyumbani, lakini baadaye alirejea.
Msuva alihitimisha karamu hiyo kwa kufunga bao la saba kwa shuti kali akimalizia mpira uliorushwa na Juma Abdul katika dakika ya 77.
Tanga, Wenyeji mabingwa wa 1988, CoastalUnion walithibitisha utu uzima dawa baada ya kuinyuka Mbeya City mabao 2-0 kwenye Uwanja wa Mkwakwani.
Mabao ya Coastal Union yalifungwa na Mohamed Mtindi katika dakika ya 79 na 89 na kuzima kasi ya Mbeya City ambayo ilitawala sehemu kubwa ya mchezo huo, lakini washambuliaji wake walikosa umakini kwenye umaliziaji.
Katika mchezo mwingine Mtibwa Sugariliichapa Ashanti United 2-1, mabao ya Mohamed Mkopi na Abdalla Juma huku Musa Mgosi akipewa kadi nyekundu.
Arusha JKT Oljoro ililoa 2-1 kutoka kwa Mgambo Shooting, huku Kagera Sugar wakiiadhibu Rhino Ranger 1-0 bao la Suleiman Kibuta.
Azam FC ina shughuli pevu leo itakapokabiliana na Prisons kwenye uwanja wake wa Azam Complex, wakati Simba itateremka kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam kupepetana na JKT Ruvu.
Ni wazi, Azam itaingia uwanjani ikiwa na mawazo ya kusaka ushindi ili kujipoza na machungu ya kutupwa nje ya Michuano ya Kombe la Shirikisho baada ya kuchapwa jumla ya mabao 2-1 na Ferroviario ya Msumbiji.
Hata hivyo, kazi haitakuwa nyepesi kwa Azam, kwani Prisons nayo imeingia mzunguko wa pili ikiwa na staili mpya ya kutoa vichapo vikali bila kujali inacheza na nani. Prisons inayokamata nafasi ya tisa ikiwa na pointi 19, haijapoteza mchezo wowote katika mechi zake tatu za mzunguko wa pili ilizokwishacheza ambapo ililazimishwa sare ya 0-0 na Coastal Union, ikaichapa Mtibwa mabao 3-1 kisha ikainyuka JKT Ruvu mabao 6-0.Nayo Simba baada ya ziara ngumu mikoani iliyoshuhudiwa ikikosa ushindi hata mmoja katika mechi zake tatu, itakuwa na fikra za kusaka ushindi ili kurejesha furaha ya mashabiki wake mbele ya JKT Ruvu.
Kocha wa Simba, Zdravko Logarusic amewaambia wachezaji wake kwamba hataki mzaha tena anahitaji ushindi tu kuanzia mchezo wa leo.
Imeandaliwa na Sosthenes Nyoni (Dar), Burhan Yakubu (Tanga), Musa Juma (Arusha), Juma Mtanda (Moro) na Phinias Bashaya (Kagera)
|
0 Comments