Rais Jakaya Kikwete, akipokea mfano wa helikopta kutoka kwa mtoto wa bilionea wa pili duniani, Warren Buffett, Howard ambaye familia yake kupitia Mfuko wa Warren Buffett Foundation watatoa helikopta moja itakayotumika kupambana na ujangili katika Pori la Akiba la Selous. Picha ya Wizara ya Maliasili na Utalii.
Dar es Salaam. Familia ya bilionea namba mbili nchini Marekani, Warren Buffett imeunga mkono juhudi za kupambana na ujangili nchini kwa kuchangia helikopta moja.
Familia ya Warren Buffett imeamua kutoa msaada huo kupitia Mfuko wa Howard Buffett Foundation, baada ya kuridhishwa na hatua mbalimbali zinazochukuliwa na Serikali.
Helikopta hiyo itatumika kwa ajili ya kusaidia mapambano dhidi ya ujangili katika hifadhi za taifa na mapori ya akiba nchini.
Msaada huo ulikabidhiwa juzi kwa Rais Jakaya Kikwete na mtoto wa bilionea huyo, Howard Buffett, ambaye yuko nchini kwa mapumziko ya kitalii.
Akikabidhi mfano wa helkopta kwa Rais Kikwete, Buffett alisema amevutiwa na kazi nzuri inayofanywa na Serikali ya Tanzania katika kukabiliana na ujangili hususan wa tembo na faru.
Waziri wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu alisema wamepokea kwa furaha ufadhili huo, ambapo utahusisha mafunzo kwa marubani wawili nchini Marekani ama Afrika Kusini kutokana na matakwa ya wizara.
“Wametuambia pesa ipo tayari ila ni jukumu letu sisi kama Serikali kuchagua aina ya helikopta tunayoitaka. Itakuwa na uwezo wa kubeba watu sita na kwa sasa tunaangalia kama tuchukue Bell ama Ecopter, wataalamu wanashughulikia,” alisema.
|
0 Comments