Mamia ya wapiganaji wa kundi la Boko Haram, wamekabiliana vikali na wanajeshi wa serikali huku milipuko na milio ya risasi ikisikika mjini Maiduguri Kaskazini Mashariki mwa Nigeria.
Wakazi wa mji huo wanasema kuwa walisikia milio ya risasi na milipuko kwa karibu saa mbili nyakati za Asubuhi.Inaarifiwa tukio hili limejiri wakati wa kile kinachoshukiwa kuwa shambulizi dhidi ya kambi ya jeshi lililofanywa na wapiganaji wa Boko Haram.

Kuna taarifa za mamia ya wapiganaji kuvamia mji huo asubuhi na mapema na kushambulia kambi mbili rasmi za jeshi ili kuwaachilia wapiganaji waliokamatwa na kuzuiliwa.
Wakazi walisema kuwa waliona ndege mbili za jeshi zikizunguka anga katika eneo hilo.
Jeshi linasema kuwa liliweza kutibua mashambulizi hayo na kusababisha majereha makubwa kwa washambuliaji hao.
Wakazi walioshuhudia makabiliano hayo walisema kuwa pande zote mbili zilipata majeraha.
Pia kumekuwa na taarifa ya milipuko kusikika ndani ya nyumba za wakazi pamoja na katika chuo kikuu cha Maiduguri.
Afisaa mkuu wa haki za binadamu katika umoja wa Mataifa Navi Pillay -- ambaye yuko nchini humo, alisema kuwa ukatili unaotendwa na wanajeshi ni sababu ya kundi la Boko Haram kuendeleza mashambulizi.
Maelfu ya watu wameuawa nchini Nigeria katika kipindi cha miaka mitano tangu kundi la Boko Haram lilipoanza vita.
Ghasia hizi zimekithiri katika miezi michache iliyopita, licha ya juhudi za maafisa wa usalama kudhibiti usalama.