Magari yakiwa katika foleni Barabara ya Mandela, eneo la Tabata Dampo jijni Dar es Salaam juzi. Picha na Salim Shao
Dar es Salaam.
Mkurugenzi wa Jiji la Dar es Salaam, Wilson Kabwe amesema Jiji la Dar es Salaam lilipangwa mwaka 1912 na haliendani na ukuaji wa kiuchumi na ongezeko la watu.
Amesema kutokana na mabadiliko hayo, ofisi yake ipo katika mikakati ya kujenga miji mingine nje ya Jiji la Dar es Salaam ili kupunguza msongamano.
“Jiji hili lilipangwa mwaka 1912, sasa hivi kuna mabadiliko makubwa ndiyo maana tunaunda miji kama Kigamboni ili kuboresha jiji lililopo,” alisema Kabwe.
Taarifa kutoka Taasisi ya Wahandisi Tanzania (IE) zinaeleza kuwa, kwa kuwa msongamano wa magari unatajwa kuwa ni dalili za ukuaji wa uchumi na kwa kuwa watu wengi wanakimbilia mijini, hivyo halina dawa.
Inaeleza kuwa sehemu kuu ya huduma kama vile soko kuu la biashara zipo Kariakoo wakati huduma za kiofisi za Serikali kwa maana ya wizara zipo maeneo ya Posta.
Mtaalamu wa Mazingira kutoka Chuo Kikuu cha Ardhi, Dk Robert Kiunsi katika utafiti wake kuhusu ‘Msongamano wa magari Dar es Salaam na mpangilio wa Jiji’ amesema kwa jumla ujenzi wa Mji wa Dar es Salaam hauna mpangilio bora.
Ripoti ya utafiti wake inaeleza zaidi kuwa, hivi sasa Jiji la Dar es Salaam lina idadi ya watu inayozidi milioni nne ambapo kati ya hao, asilimia 60 wameajiriwa katika sekta rasmi ikiwamo biashara, uvuvi, kilimo, kazi za viwandani, useremala na uashi, hivyo wote hufanya kazi katika eneo moja.
Wakati huohuo, Takwimu kutoka Chuo Kikuu cha Ardhi zinaeleza kuwa, asilimia 60 hadi 75 ya wakazi wa Jiji la Dar, wanaishi katika makazi holela. Alisema asilimia 78 zilizobaki ni eneo lililojengwa bila mpangilio au halijajengwa na limefunikwa na uoto wa asili au kilimo.
Katika asilimia 21.7 ya maeneo yaliyojengwa kwa mpango, eneo la makazi ni asilimia 13.2, vyanzo vya maji asilimia 4, viwanda 1.3 na taasisi za Serikali ni 3.2.
Ripoti hiyo ilieleza kuwa hata ujenzi wa miundombinu ya barabara unachangia msongamano kwa mfano ujenzi wa barabara za Jiji la Dar es Salaam umejikita katika barabara tano zinazoelekea kwenye njia kuu ambazo ni Kilwa, Nyerere, Bagamoyo na Morogoro pamoja na barabara kuu moja ambayo ni Mandela.
Hata hivyo, urefu wa barabara zote hizi ni sawa na kilometa 1,717 ambazo ni asilimia 23 tu zimejengwa kwa kiwango cha mawe au changarawe.Ongezeko la watu litachochea ukuaji wa mahitaji na shughuli za kiuchumi hivyo mahitaji ya miundombinu yatakuwa makubwa zaidi na msongamano utakithiri zaidi.
Ripoti hiyo inaeleza kuwa msongamano wa magari unatokana na sababu nyingi ikiwamo, ukuaji wa uchumi, ongezeko la magari, mpangilio mbovu wa jiji, miundombinu duni, kukosa mpangilio wa mji ulioboreshwa na ongezeko kubwa la watu mijini.
Tayari Serikali ipo katika hatua ya mwisho ya kuandaa mpango mji mpya wa jiji (2012-2032). Baadhi ya mapendekezo yake yameshaanza kutekelezwa ukiwamo Mradi wa Mabasi Yaendayo Kasi wa Dart.
Meneja Mawasiliano wa Mamlaka ya Usafiri Nchi Kavu na Majini (Sumatra), David Mziray alisema mpaka mwaka jana Julai, kulikuwa na pikipiki laki sita, huku jumla ya vyombo vyote vya moto vikiwa ni 1,200,000.
Alisema ongezeko la magari ni miongoni mwa sababu za msongamano wa magari jijini, lakini alisema Sumatra walitoa suluhisho la kuzuia pikipiki na magari madogo (vipanya) visiingie katikati ya mji na badala yake mabasi makubwa yanayobeba abiria wengi ndiyo yanayoruhusiwa.
Mziray aliongeza kuwa suluhisho la kupunguza msongamano ni kuboresha miundombinu ya barabara na kujenga miji kwa mipango.
|
0 Comments