Na Saleh Ally, Cairo
MABINGWA wa Tanzania Bara, Yanga, wanaondoka leo kwenda mjini Alexandria kwa ajili ya mechi ya kesho dhidi ya Al Ahly ambao wana mbinu nyingi za nje na ndani ya uwanja.
Hakuna ubishi mechi ni ngumu, lakini Yanga wakijipanga, wakatulia na kufanya wanachotaka kukifanya, huenda kikawa ni kiama cha Waarabu hao wanaoongoza kwa kuchukua makombe ya kimataifa kuliko klabu yoyote duniani.
Mechi ya kwanza, Yanga ilishinda kwa bao 1-0 nyumbani Dar es Salaam, mechi ya kesho itapigwa kwenye Uwanja wa Alex mjini humo, saa 1 usiku ambayo ni saa 2 usiku nyumbani.
Mechi hiyo haitakuwa na mashabiki na imefanyika hivyo kutokana na hofu ya kuzuka kwa vurugu tena kama ilivyokuwa katika mechi ya mwisho ya Ahly walipoifunga CS Sfaxien ya Tunisia na kutwaa ubingwa wa Super Cup jijini hapa.
Haitakuwa kazi rahisi, lakini kikosi cha Yanga kinaonekana kipo fiti na tayari kwa ajili ya mchezo huo na wenyeji wameonyesha hofu, maana yake watakuwa wameongeza umakini.
Tokea Yanga imetua hapa Alhamisi alfajiri, tayari imefanya mazoezi mara tatu. Mara moja Alhamisi usiku, mara mbili Ijumaa asubuhi na usiku.
Kocha Mkuu, Hans van Der Pluijm, anaamini kikosi chake kiko fiti na wako tayari kwa mchezo, lakini amesisitiza haiwezi kuwa mechi lelemama na kila mchezaji atatakiwa kufuata maelekezo atakayopewa kwa asilimia mia.
“Kama wataelewa na kufuata maelekezo kwa asilimia mia, hakuna shaka tutafanya vizuri. Ahly wana mbinu nyingi, ni wajanja na wanafanya mambo kwa uwezo na hila, ilimradi washinde.
“Tumezungumza karibu kila kitu, mbinu zao, uchezaji wao, aina ya kushambulia, aina ya kujilinda. Hatujaanza leo lakini tunakumbusha kila kitu,” alisema Pluijm.
Kuhusiana na suala la mechi hiyo kuhamishiwa mjini Alexandria, Pluijm alisisitiza bado wako tayari na anajua hizo ni sehemu za mbinu za Al Ahly.
“Sisi kama wachezaji tunabaki na hisia za uwanjani. Kokote watakapotaka, basi tutacheza, tunachotaka ni kusonga mbele” alisema kocha huyo wa zamani wa Berekum Chelsea ya Ghana.
“Tunajua wana baadhi ya wachezaji ambao atacheza, lakini najua kuna baadhi ya wachezaji ni majeruhi. Sitaki kuangalia sana hilo, najua wana mbinu nyingi. Lakini kikubwa ni siku tutakapokuwa uwanjani.
“Katika soka, mambo ya mazoezi na yale ya uwanjani wakati mwingine yanapishana. Lakini ninaamini mambo yatakwenda vizuri,” aliongeza.
Yanga imekuwa ikijiandaa na krosi mbaya za Ahly, ushambuliaji wao wa kasi, pia tabia ya kujiangusha ya wachezaji wa timu hiyo.
Ingawa Yanga ilitawala mchezo wa Dar es Salaam, lakini ilishindwa kuzitumia nafasi ilizozipata kufunga mabao zaidi.
“Kweli hatukuzitumia nafasi hizo, lakini safari hii hatutakuwa na nafasi nyingi lakini nimewaambia zile chache tutakazotengeneza, basi zitumike,” alisema.
Kuhusu hali ya hewa, Pluijm aliongeza: “Hali ya sasa ni nzuri tu, si kama kipindi kile Charles (Mkwasa) alipokuja huku. Tunaweza kucheza tena vizuri tu.”
|
0 Comments