Stori: Makongoro Oging’ na Imelda Mtema
NI balaa ni nini? Mariam Athuman Sepetu ambaye ni mama mzazi wa Miss Tanzania 2006, Wema Sepetu ametinga katika Kituo cha Polisi Kijitonyama ‘Mabatini’, Dar kutoa taarifa ya kupotelewa hati ya uthibitisho ya kifo cha mume wake, marehemu Isaac Sepetu.Vyanzo vyetu toka ndani ya jeshi la polisi vinasema kwamba, mama Wema alifika kituoni hapo Machi 19, mwaka huu na kutoa taarifa hiyo yenye kumbukumbu KJN/RB/2499/2014 na alihofu kuwa huenda hati hiyo iliibwa na wajanja wenye nia mbaya.

Ilidaiwa kuwa siku ya tukio saa nne usiku, mama huyo aliitafuta hati hiyo ili kesho yake akafungue madai ya mirathi ya mumewe lakini hakuiona mahali alipoiweka jambo lililomfanya aende polisi kuwajulisha.
Hati hiyo, kwa mujibu wa chanzo cha kipolisi  hati hiyo ilitolewa katika Hospitali ya TMJ jijini Dar, Oktoba 27, mwaka jana.
Jumapili iliyopita, Uwazi lilimtafuta mama huyo ili kujua kama yeye ndiye aliyefikisha taarifa hizo polisi.
“Nililazimika kwenda huko kwa sababu hiyo ndiyo njia pekee na sikuweza kujua kama aliyeichukua alikuwa na nia gani, lakini hata hivyo baada ya siku kadhaa kupita tangu nitoe taarifa niliitafuta tena nikakuta imerudishwa,” alisema mama Wema.