Mwenyekiti wa muda wa Bunge la katiba Pandu Kificho akitoka katika ukumbi maalumu wa bunge la katiba mjini Dodoma. Picha na Maktaba 
Geita.
 Viongozi na jamii nchini wametakiwa kuwa makini na vyama vya siasa na makundi yanayoibuka ndani ya Bunge la Katiba kwa lengo la kupindisha maoni yaliyotolewa.
Badala yake wametakiwa kusimama kwenye mstari na kuwatetea wananchi, kwani wao ndiyo wawakilishi wao kwenye Bunge hilo.
Hayo yalisemwa jana na Askofu wa Jimbo Katoliki la Geita, Damian Dallu wakati wa iliyofanyika katika Kanisa Katoliki la Bikira Maria wa Fatima. Hivi sasa Bunge la Katiba linakabiliwa na wakati mgumu kutokana na msuguamo miongoni mwa wajumbe juu ya mfumo sahihi wa upigaji kura.
“Hakika kuna watu wanaibuka, wanapinga  baadhi ya maoni yalitolewa na wananchi na wengine wanaleta maoni mapya,” alisema.
Dallu alisema inasikitisha kuona kuna baadhi ya wajumbe wako bungeni kwa ajili ya masilahi binafsi na siyo kwa niaba ya wananchi.
Alisema vitendo hivyo ni hatari kwa taifa na jamii, hivyo haipo sababu ya viongozi kufumba macho dhidi ya watu wachache wenye tabia za kutaka masilahi binafsi.
“Amani inalindwa na katiba ya nchi, kama tukiharibu katiba basi tufahamu kwamba tumeharibu amani ya taifa.
Viongozi wote wa dini tuliombee Bunge hili ili Mungu aliepushe na watu wenye maoni binafsi kwa masilahi yao,” alisema zaidi Dallu.
Kadhalika, Askofu Dallu alihimiza jamii kuridhika na mali walizonazo hata kama ni kidogo.“Lazima kufanya kazi kwa bidii ili tuepuke tabia ya kuwa ombaomba. Tukitaka pesa za haraka haraka, ni rahisi kuingia kwenye dhambi,” alisema Dallu.
Aliwaonya viongozi wa Serikali kuepuka kutumia udhaifu wa umaskini wa taifa kwa kujiingiza kwenye sera za kuomba kutoka mataifa ya nje.