Rais Obama akiwa wa Waziri Mkuu wa Ukraine
Rais wa Marekani Barrack Obama, ameonya Urussi kusitisha mpango wake wa kutaka kutwaa eneo la Crimea nchini Ukraine lasivyo iwekewe vikwazo.
Akiongea katika Ikulu ya White House baada ya kufanya mashauriano na kaimu Waziri Mkuu wa Ukraine, Arseniy Yatsenyuk, rais Obama amesema nchi moja haiwezi kulazimisha taifa lingine kwa mtutu wa bunduki.
Bwana Yatsenyuk amesema taifa lake sasa ni sehemu ya mataifa ya Magharibi na kamwe haliwezi kurudi nyuma.

Mabalozi katika Umoja wa Mataifa, wanasema Mataifa ya Magharibi yanaandaa azimio la pamoja, katika baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa ambalo litakariri uhuru wa taifa la Ukraine na pia kuangazia kuhusu kura ya maoni kuhusu itakayofanyika siku ya Jumapili, ikiwa eneo hilo la Crimea litajitenga na kuwa sehemu ya Urussi.
Hata hivyo inatarajiwa kuwa Utawala wa Moscow utatumia kura yake ya turufu katika baraza hilo la Umoja wa Mataifa kupinga azimio hilo.