Rais wa Tanzania Jakaya Kikwete akifafanua jambo. Picha na Maktaba 
Dar es Salaam. Jana katika gazeti hili tulichapisha habari iliyokuwa ikielezea kuwa Rais Jakaya Kikwete aliwatembea wagonjwa katika Taasisi ya Tiba ya Mifupa na Upasuaji wa Mishipa ya Fahamu (MOI) jijini Dar es Salaam.
Katika habari hiyo tuliwataja aliowatembelea kuwajulia hali kuwa ni Rajab Maranda, ambaye anatumikia kifungo cha miaka 18 jela kwa wizi wa fedha katika Akaunti ya Madeni ya Nje (EPA), pamoja na mwandishi wa Kituo cha Televisheni cha Channel Ten, Salum Mkambala.
Hata hivyo, taarifa iliyotolewa jana na Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais imeeleza kuwa Rais Kikwete hakwenda kumuona Maranda bali aliwatembelea wanahabari wawili ambao ni Salum Mkambala wa Channel Ten aliyelazwa wodi binafsi D, na Margaret Chambiri wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi aliyelazwa wodi binafsi .
Taarifa hiyo pia inaeleza kuwa Rais Kikwete aliwajulia hali wagonjwa wengine wawili, John Mhina na Reuben Nyanga ambao wako chumba kimoja na Mkambala.
Tunachukua nafasi hii kuomba radhi kwa Rais Kikwete kwa usumbufu ambao ameupata kutokana na habari hiyo.
Mhariri