Na Waandishi Wetu AMA kweli ajuaye siku ya binadamu kufa ni Mungu peke yake, kama wanadamu nao wangepewa uwezo huo, kuna mipango ingekuwa haipangwi kwa kujua haitatimia, ndivyo ilivyotokea kwa marehemu Muhidin ‘Maalim’Gurumo ambaye ameaga dunia akiwa na zawadi aliyotaka kumpa Mbongo-Fleva, Nasibu Abdul ‘Diamond Platinumz’.
Gurumo alifariki dunia Aprili 13, 2014 katika Wadi ya Mwaisela Hospitali ya Taifa Muhimbili jijini Dar na kuzikwa Aprili 15, mwaka huu kwenye Makaburi ya Kijiji cha Masaki, Kisarawe mkoani Pwani.
Zawadi ambayo marehemu Gurumo alikuwa ampatie Diamond ni mashairi ya wimbo ambao upo tayari na sasa, ilikuwa wakutane na kukabidhiana tu.
ILIKUWA HIVI Kwa mujibu wa Meneja wa Diamond, Babu Tale ambaye alizungumza na Amani juzi msibani nyumbani kwa Gurumo, Mabibo jijini Dar, Ijumaa ya Aprili 11, mwaka huu, mzee huyo alimpigia simu ya mkononi yeye (Babu Tale) baada ya kumkosa Diamond.
“Aliniuliza mwanangu (Diamond) yuko wapi? Nikamwambia
yuko nje ya nchi. Akaniambia nina zawadi nzuri sana nataka kumpa kabla sijafa.“Nilimuuliza ni zawadi gani? Akasema ametunga wimbo, tayari umekamilika sasa anataka kumpa aimbe yeye mwenyewe (Diamond) au waimbe wote.
“Niliona ni wazo zuri sana, nikamwambia kwa sababu Diamond atarudi Jumapili, basi Jumatatu tutakuja, akasema sawa asikose. Sikujua kama anaumwa, sikujua kama anazungumza na mimi maneno ya mwisho,” alisema Babu Tale ambaye kwa kiasi kikubwa ameshiriki kumwinua kisanii Diamond.
DIAMOND APIGIWA SIMU, AFURAHIA Babu Tale aliendelea kusema kuwa, baada ya kumaliza kuzungumza na mzee Gurumo alimpigia simu Diamond ambapo alimwambia kilichosemwa na mzee huyo.
“Nilimpigia simu Diamond baada ya kukata kwa mzee Gurumo, nikamwambia alichosema mzee wake. Sikujua kama Diamond angefurahi sana, lakini kusema kweli alifurahi sana tena sana akasema mzee ametoa wazo zuri ambalo litamwingiza kwenye historia nyingine kwa vile atakuwa ameimba na mkongwe wa muziki Tanzania.
DIAMOND ASHTUKA, AKIONA KIFO CHA GURUMO Babu Tale akaendelea: “Lakini cha ajabu, Diamond akawa kama ameshtuka, akasema da! Huyo mzee ametoa wazo zuri namna hiyo? Au anataka kufa nini?”
Meneja huyo aliendelea kusema kuwa, baada ya hapo hakuwa na mawasiliano tena na mzee Gurumo hadi Jumapili, siku mbili mbele baada ya tamko la kumpa Diamond zawadi ya wimbo ambapo alipigiwa simu na mtu akimwambia mzee Gurumo amefariki dunia.
Anasema: “Najua Gurumo alitaka kumpa Diamond wimbo huo kama zawadi yake na yeye kufuatia Diamond kumzawadia gari (Toyota FunCargo) alilomkabidhi mwaka jana kwa ‘kumsapraizi’.”
JINA LA WIMBO Babu Tale hakutaja jina la wimbo huo lakini fukuafukua ya Amani iliambiwa kuwa, wimbo ambao Gurumo alitaka kumpa Diamond unaitwa Shukurani kwa Mtoto.
Amani lilifanya jitihada za kuzungumza na mtoto yeyote wa marehemu ili kujua kama kuna mwenye kuelewa kuhusu wimbo huo na kama mashairi yake yanaweza kupatikana, lakini bila mafanikio baada ya watoto wote kuwa katika majonzi yasiyopimika kwa kiwango cha macho ya kibinadamu.
DIAMOND AANGUA KILIO KAMA MTOTO Habari nje ya Babu Tale zinadai kuwa, Diamond alipojulishwa juu ya kifo cha mzee Gurumo aliangua kilio kama mtoto mdogo.
Inadaiwa kuwa, staa huyo aliyekuwa nchini Nigeria kwa shoo kadhaa, alikuwa akilia huku akikumbuka maneno ya Babu Tale kuhusu kuimba wimbo na mzee huyo ambaye Jumatatu ya kukutana kwao ndiyo mwili wake ulikuwa Mochwari ya Hospitali ya Muhimbili jijini Dar.
“Diamond alilia huku akisema kuwa ameikosa bahati moja kubwa sana na hatakuja kuipata tena katika maisha yake. Unajua yeye alikubali wazo la Gurumo akijua ni ‘kiki’ ya kuendelea kufanya vyema kwenye gemu,” kilisema chanzo kimoja.
Jitihada za kumpata Diamond ambaye alikosa kuhudhuria mazishi ya mzee Gurumo zilishindikana baada ya simu yake ya kiganjani kuita bila kupokelewa. Hata alipotumiwa ujumbe mfupi hakuujibu.
GURUMO ANAHITIMISHA SAFU YA WAIMBAJI MSONDO Kifo cha Maalim Gurumo kinahitimisha safu ya waimbaji wakongwe wa kwenye Bendi ya Msondo Music. Waimbaji wengine waliotangulia mbele ya haki ni Suleiman Mbwembwe, TX Moshi William, Athuman Momba na Joseph Maina.
Wote hawa ndiyo walioimba wimbo maarufu wenye mashairi yasemayo ‘tunatoana roho yarabi iii…kwa mali alizoacha baabaa’... Ukiiangalia video ya wimbo huo, waimbaji wote ni marehemu. Inauma sana! Marehemu Gurumo alizikwa juzi `Jumanne kwenye Makaburi ya Kijiji cha Masaki, Kisarawe Pwani.
Mungu ailaze roho yake mahali pema peponi. Amina.
|
0 Comments