Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), Jaji mstaafu Damian Lubuva.PICHA|MAKTABA
Bagamoyo. Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), Jaji mstaafu Damian Lubuva amesema vituo vya kupigia kura katika Uchaguzi Mkuu wa 2015 vitaongezeka mara mbili zaidi ya vile vilivyotumika katika uchaguzi uliopita. Jaji Lubuva alisema hatua hiyo ni mojawapo ya njia za kukabiliana na changamoto ya Watanzania wengi kutokushiriki katika uchaguzi kutokana na umbali wa vituo. Alitoa kauli hiyo jana wakati akifungua mafunzo ya wiki mbili kwa watumishi 20 (15 Bara na watano Zanzibar), mjini Bagamoyo yenye lengo la kuwaongezea uwezo wa kukabiliana na changamoto ambazo hujitokeza nyakati za uchaguzi mkuu. “Mchakato wa daftari kwa sasa umefikia kwenye hatua nzuri, tunajiandaa kupata vifaa lakini idadi ya vituo itakuwa zaidi ya 40,000 ukilinganisha na takriban 20,000 vya mwaka 2010. Hii itasaidia kushawishi Watanzania kujitokeza kwenda kupiga kura,” alisema Jaji Lubuva na kuongeza:“Changamoto nyingine ni elimu ndogo kwa wapigakura wanaohama eneo moja kwenda jingine bila kufuata utaratibu, matokeo yake wanakosa haki ya kupiga kura.” Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC), Salim Jecha Salim alisema imani ndogo ya matokeo miongoni mwa wanasiasa imekuwa ni moja kati ya changamoto kubwa inayowasumbua katika nafasi zao.“Hiyo ni changamoto ambayo imekuwa ikijitokeza mara kwa mara katika chaguzi, wengi wamekuwa hawana imani kabisa na matokeo tunayokuwa tunatoa katika kipindi cha uchaguzi, hivyo tunachokifanya ni kuwaelimisha Watanzania,” alisema Salim.