Waziri wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu akiwaonyesha watalii bilionea kitabu chenye maelezo ya vivutio vya utalii nchini. Picha na Peter Saramba
Arusha. Watalii bilionea 100 kutoka nchi za Ulaya na Marekani wanaotumia ndege binafsi aina ya Boeing BBJ 737 HB-11Q wametembelea Hifadhi ya Taifa ya Serengetina kuisifia, wakisema ni moja ya urithi wa dunia unaostahili kutunzwa kwa faida ya vizazi vya sasa na vijavyo.
Watalii hao walioingia nchini Machi 28, mwaka huu wakiongozwa na Mwanzilishi na Mwenyekiti wa Kampuni ya Abercombie & Kent, Geoffrey Kent, jana walikutana na Waziri wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu aliyefika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa waKilimanjaro kuagana nao.
Mbali na Tanzania, mabilionea hao wanaozunguka dunia pia watatembelea nchi za Italia, Botswana, Malawi, Zambia, Uganda, Namibia, Ethiopia na Afrika Kusini.
Kundi la kwanza la matajiri hao liliingia nchini Machi 8, mwaka huu likifuatiwa na kundi la pili lililoingia Machi 28, mwaka huu na kutembelea Hifadhi ya Serengeti kwa siku tatu.
“Nilifika Hifadhi ya Serengeti miaka ya sitini nikiwa kijana mdogo, lakini nimerejea nikiwa mzee na kukuta mazingira na uasilia wa hifadhi ukiwa vilevile,” alisema Kent.
Aliongeza: “Ni jambo linalotia faraja kwa sekta ya uhifadhi duniani, lazima tuendelee kuhifadhi Serengeti ili kuilinda kwa faida ya vizazi vijavyo.”
Akikabidhi zawadi ya majarida na vitu mbalimbali vinavyotangaza vivutio vya utalii nchini, Waziri Nyalandu alisema ujio wa watalii hao matajiri ni faraja kwa sekta ya utalii, kwani ziara yao itajenga imani kwa wenzao ambao hawajafika nchini kutembelea vivutio vya utalii.
“Sekta ya utalii huchangia asilimia 17 ya pato la taifa. Lengo letu ni kuhakikisha sekta hiyo inachangia asilimia 25,” alisema Nyalandu.
Kwa mujibu wa takwimu za Wizara ya Maliasili na Utalii, zaidi ya watalii milioni 1.7 walitembelea nchini mwaka jana, huku lengo la mwaka huu likiwa watalii milioni 2.
Nyalandu alisema ili kufikia lengo hilo, Serikali inakusudia kuhamasisha utalii wa makundi kwa kutumia ndege binafsi na mabasi kulingana na uwezo wa watalii wenyewe.
“Utalii wa makundi umeleta faida kubwa nchini, sasa Serikali inakusudia kufungua milango zaidi ya kuhamasisha ili wengi waje kutembelea hifadhi zetu,” alisema Nyalandu.
Baada ya kusikia kauli ya Nyalandu, Kent aliahidi kuwa balozi wa kutangaza Sekta ya Utalii Tanzania kwenye nchi zote za Ulaya na Marekani.