Muuza magazeti katika eneo la Posta ya Zamani akiyapanga magazeti yake chini baada ya meza aliyokuwa akiitumia kuvunjwa na Askari wa Jiji wanaoendelea na Operesheni Safisha Jiji la Dar es Salaam, jana. Picha na Joseph Zablon
Dar es Salaam. Wauza magazeti wa jijini Dar es Salam wamelalamikia operesheni ya kusafisha jiji iliyotekelezwa na askari wa halmashauri ya jiji, wakieleza kwamba haikuwatendea haki kwa kuharibu mali zikiwamo meza na magazeti ambazo zilisombwa na askari hao waliosindikizwa na askari wa Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU).
Wakizungumza jana kuhusu operesheni hiyo ya jiji iliyoanza juzi kutekelezwa mitaa mbalimbali , wafanyabiashara hao walisema kuwa waliharibiwa magazeti na meza zao zilizokuwa na nembo za kampuni mbalimbali ikiwamo Mwananchi Communications Ltd inayochapisha gazeti hili, Mwanaspoti na TheCitizen, ambapo baadhi yao wamekamatwa na kufikishwa mahakamani.
“Jana (juzi) hawakuuliza vibali, wala kitu kingine cha namna hiyo zaidi ya kudai kuwa hatutakiwi kuweka meza, labda tupange chini na ndiyo maana unaona leo wengi wamepanga magazeti chini badala ya mezani,” alisema Salum Ramadhani wakala wa magazeti eneo la Printpak kwa niaba ya wenzake.
Akizungumza ofisini kwake jana, Ofisa Uhusiano wa Manispaa ya Ilala, Tabu Shaibu alisema kuwa kila muuza magazeti anatakiwa awe na kibali kutoka ofisi ya mtendaji wa kata anayokusudia kufanya.
“Ndiyo utaratibu kila muuza magazeti kuwa na kibali cha mtendaji wa kata lengo ni kujua idadi yao na kutengewa au kuruhusiwa kufanya biashara katika eneo ambako huduma hiyo hakuna na sio kama ilivyo sasa.”
Jiji jana liliendesha operesheni ya kusafisha jiji ambapo walibomoa mabanda kadhaa ya biashara na kuwakamata baadhi yao na kuna ambao wamefikishwa mahakamani na mpango huo unatajwa kuwa ni endelevu kuhakikisha kuwa jiji linakuwa safi.