Lanjui aliyelazwa katika Wodi Namba Nne katika hospitali hiyo tangu Januari Mosi, 1971, awali alilazwa katika Hospitali ya Sekou Toure, Mwanza kuanzia mwaka 1969 mara baada ya kupata ajali.PICHA|MAKTABA 

Singida.
 Usiombe yakupate. Abdi Lanjui (75), ametimiza mwaka wa 45 akiwa wodini katika Hospitali ya Mkoa wa Singida alikolazwa tangu mwaka 1971 baada ya kupata ajali ya lori.
Lanjui aliyekuwa dereva wa taasisi aliyoiita “Mamlaka ya Pamba,” alipata ajali hiyo mkoani Mwanza baada ya lori alilokuwa akiendesha kuchomoka gurudumu la mbele na kupinduka.
“Sababu ya mimi kugeuza wodi kuwa makazi yangu ya kudumu ni ajali iliyosababisha kupooza kuanzia kiunoni hadi kwenye nyayo. Kwa kuwa sinyanyuki kitandani, nimepata vidonda kuanzia makalioni hadi miguuni. Kwa sasa naishi maisha magumu mno,” alisema.
Aomba msaada
Kutokana na hali hiyo, ameiomba Serikali na jamii kwa jumla kumsaidia chakula kwa kuwa hana ndugu wa kumsaidia. Lanjui ambaye hawezi kunyanyuka kitandani, alisema kwa miaka mingi uongozi wa hospitali ya mkoa ulikuwa ukimhudumia kwa kumpa chakula lakini baadaye huduma hiyo ilisitishwa, hivyo kumfanya awe ombaomba na maisha yake kuwa ya mlo mmoja kwa siku.
“Kwa vile siwezi kunyanyuka kitandani na sina ndugu yeyote, nimekuwa nikiwaomba msaada manesi na watumishi wengine wa hapa hospitali. Nashukuru sana wamekuwa wakinisaidia bila kuchoka na kuniwezesha kupata walau mlo wa siku moja,” alisema. Lanjui ambaye anazungumza vizuri pia aliomba msaada wa fedha za kwenda Hospitali ya KCMC, Moshi ili apatiwe huduma zaidi ya matibabu.
Mwanza hadi Singida
Lanjui aliyelazwa katika Wodi Namba Nne katika hospitali hiyo tangu Januari Mosi, 1971, awali alilazwa katika Hospitali ya Sekou Toure, Mwanza kuanzia mwaka 1969 mara baada ya kupata ajali.
Alisema akiwa Sekou Toure mwishoni mwa mwaka 1970, hali yake ilibadilika na kuwa mbaya ndipo alipomwomba mwajiri wake amrudishe nyumbani katika Kijiji cha Mhintiri katika Wilaya ya Ikungi mkoani Singida ili ‘akasubiri kifo chake.’
Hata hivyo, alisema uongozi wa Mamlaka ya Pamba ulikataa kumpeleka kijijini kwake, badala yake ulimkabidhi katika Hospitali ya Mkoa wa Singida mwaka 1971.
Alisema wakati anapata ajali na kulazwa hospitalini, wazazi na ndugu yake wa pekee, walikuwa wamekwishafariki dunia.
Kaimu Mganga Mkuu wa hospitali hiyo, Mussa Kamala alisema hivi sasa mgonjwa huyo anahudumiwa na hospitali kama watu wengine wenye ulemavu ambao hawatozwi gharama yoyote.Alisema uongozi wa hospitali uliwahi kumkabidhi kwa Idara ya Ustawi wa Jamii ili ifanye mipango ya kumrudisha nyumbani, lakini haikuwezekana. Ofisa Ustawi wa Jamii Mkoa wa Singida, Zuhura Kalya alisema walishindwa kumrejesha kwao kwani walipofuatilia ilibainika kuwa hana ndugu na hakukuwa na mtu anayemfahamu kwa sababu aliondoka kijijini hapo mwaka mmoja baada ya uhuru.