Waombolezaji wakimfariji Leticia Filbert, mke wa daktari bingwa wa Hospitali ya Temeke, marehemu Dk Gilbert Buberwa nyumbani kwake Kinyerezi, Dar es Salam jana. Picha na Salim Shao 


Dar es Salaam. 
Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Akili nchini, Gilbert Buberwa amefariki dunia kutokana na ugonjwa wa dengue.
Kifo cha Dk Buberwa kinafanya idadi ya watumishi wa afya waliofariki dunia kutokana na ugonjwa huo kufikia wawili baada ya muuguzi Hamida Likoti kufariki dunia wiki iliyopita.
Ugonjwa huo uliolipuka mkoani Dar es Salaam, umezua taharuki kwa wakazi wake kwa sababu hauna tiba na unasababishwa na mbu, Aedes Egyptae, anayeuma mchana na anayeweza kuzaliana katika majisafi yaliyotuama.
Rais wa Chama cha Madaktari Tanzania (MAT), Dk Primus Saidia alisema jana kuwa Dk Buberwa alifariki dunia saa saba usiku wa kuamkia jana akiwa katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH).
Dk Buberwa alianza kuumwa ugonjwa huo akiwa kazini katika Hospitali ya Temeke na kulazwa na hali yake ilipobadilika, alihamishiwa MNH kwa matibabu zaidi.
“Kadiri siku zilivyozidi kwenda alibainika kwamba viungo vyake muhimu, yaani ini na figo vimeharibika, hivyo alisafishwa figo huku akiwa amelezwa Chumba cha Uangalizi Maalumu (ICU).
Dk Saidia alikumbusha kuwa virusi vya dengue havina tiba isipokuwa dalili zake ambazo ni homa, kuumwa kichwa na viungo vya mwili – ndizo zenye tiba.
Dk Buberwa alianza kuugua Mei 3, mwaka huu na siku iliyofuata alipelekwa hospitali na mkewe ambako alilazwa ili kupata uangalizi wa karibu wa madaktari wenzake.
Kaka wa marehemu, Wakili Nickson Ludovick alisema: “Tunasubiri ndugu kutoka Bukoba na Musoma kwa mazishi yatakayofanyika hapa Dar es Salaam katika makaburi ya Kinyerezi keshokutwa.”
Madaktari, wauguzi walazwa
Dk Malima alisema hadi jana, wafanyakazi tisa wa Hospitali ya Temeke walikuwa wamelazwa kutokana na homa hiyo.
Alisema wafanyakazi hao ni madaktari watano, wauguzi watatu na mtaalamu mmoja wa maabara. “Kwa kipindi cha wiki mbili zilizopita tumepokea wagonjwa wa dengue waliothibitika 15,” alieleza Dk Malima.