Amanda Spencer amehukumiwa kwa kuwauza watoto katika biashara ya ngono
Mwanamke aliyekuwa kinara wa mtandao uliokuwa unawaingiza watoto wadogo katika biashara ya ngono amehukumiwa kifungo cha miaka 12 jela nchini Uingereza.
Inaarifiwa Amanda Spencer, alifanya urafiki na wasichana hao wadogo wengine wakiwa na umri wa miaka 13 kabla ya kuwalazimisha kufanya ngono na wanaume na kisha kuwalipa.Mahakama ya Shefield iliambiwa kuwa Amanda alitumia pesa zake kwa madawa ya kulevya na pombe.

Spenser mwenye umri wa miaka 23, alipatikana na hatia wiki jana kwa makosa 16 yote yakihusishwa na biashara ya ngono kwa watoto wadogo.
Hata hivyo mahakama ilifutilia mbali makosa mengine 7 dhidi yake ikiwemo, kupanga na kufanikisha biashara ya ngono miongoni mwa watoto, kuwalazimisha watoto kuwa makahaba na kuwatumia vibaya watoto.
Wakati wa kesi hiyo, mahakama iliarifiwa kuwa Spencer aliwalenga watoto ambao walikuwa hawana uwezo.
Lakini Spencer alikana mashitaka yote dhidi yake akisema kuwa waathiriwa walisema uongo na kwamba hajawahi kukutana nao wala hawafahamu.
Alishitakiwa pamoja na wanaume wengine wanne, lakini watatu waliachiliwa huku mshitakiwa mwenza mwenye umri wa miaka 68 Ian Foster akipatikana na hatia.Foster alifungwa jela miaka 14 baada ya kupatikana na hatia ya makosa 12 ikiwemo kuwadhulumu watoto wadogo.
Foster alipatikana na hatia ya kuwadhulumu kingono wasichana wadogo wengine wakiwa na umri wa miaka 12.
Mahakama iliarifiwa kuwa Kawaida Bwana Foster, aliwapeleka wasichana hao katika kumbi za burudani na kuwatumbuiza kabla ya kwenda nao nyumbani kufanya nao mapenzi pia aliwanunulia pombe na sigara ili kuwalewesha kabla ya kuwadhulumu.
Baada ya hukumu polisi walisema kuwa hukumu hizo zilitokana na uchunguzi wa miaka miwili katika vitendo vya dhuluma za kingono dhidi ya watoto kati ya mwaka 2004 na 2011.
Maafisa walianza kuwa na wasiwasi kuhusu hali ya wasichana hao ambao walikuwa wanatoweka wasijulikane waliko na hivyo kulazimika kuanzisha uchunguzi mwaka 2011.