Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Mhe. Maalim Seif Sharif Hamad, akikabidhi kompyuta kwa Mkurugenzi Mkuu wa Jumuiya Al-Noor Charitable Agency, Sheikh Nadir Mahfoudh nyumbani kwake Mbweni, kwa ajili ya Radio Al-Noor ilipata ajali ya kuungua moto mwezi April mwaka huu. Wengine ni baadhi ya viongozi wa Jumuiya hiyo. (Picha na Salmin Said, OMKR)

 Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Mhe. Maalim Seif Sharif Hamad, akikabidhi kompyuta kwa Mkurugenzi Mkuu wa Jumuiya Al-Noor Charitable Agency, Sheikh Nadir Mahfoudh kwa ajili ya Radio Al-Noor ilipata ajali ya kuungua moto mwezi April mwaka huu.
Na Hassan Hamad, OMKR
 
Jumuiya ya Al-Noor Charitable Agency, imesema kuwa inakusudia kuweka vifaa vya kisasa vya kudhibiti majanga ya moto kwa Radio Al-Noor FM, ili kujikinga na majanga hayo.
 
Mkurugenzi Mkuu wa Jumuiya hiyo Sheikh Nadir Mahfoudh ameeleza hayo wakati akizungumza na Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Mhe. Maalim Seif Sharif Hamad nyumbani kwake mbweni, baada ya kupokea msaada wa kompyuta mbili kwa ajili ya Radio hiyo iliyoungua moto mwezi April mwaka huu.
 
Amesema kwa sasa wanaendelea na matengenezo ya studio zilizoungua moto, lakini kwa kushirikiana na shirika la umeme Zanzibar (ZECO), wanajipanga kuweka vifaa vitakavyoweza kudhibiti majanga ya moto ambayo yamekuwa yakikikumba kituo hicho cha Radio mara kwa mara.
Amesema mbali na msaada huo wa Kompyuta, wamekuwa wakipokea misaada mbali mbali kutoka kwa wafadhili na waislamu wengine ndani na nje ya nchi, na kuleta mwelekeo mwema wa kukifufua kituo hicho kilichoungua vibaya kwa moto na kulazimika kusitisha matangazo yake.
 
Hata hivyo Sheikh Mahfoudh amesema wanatarajia kurusha tena matangazo ya Radio Al-Noor FM aliyopo Mtoni Kidatu  Zanzibar ndani ya kipindi cha siku kumi zijazo.
 
Amesema hatua hiyo imefikiwa kufuatia uamuzi wao wa kujenga studio mbili za muda, ili kuruhusu matangazo hayo, hadi hapo watakapofanya matengenezo kamili ya studio zilizoungua.
 
Amesema Radio Al-Noor ina wasikilizaji wapatao laki tatu kwa mujibu wa tafiti rasmi, na kwamba inakuwa Radio ya mwanzo  kuwa na wasikilizaji wengi zaidi kwa Radio za Kiislamu Zanzibar.
 
Amewashukuru waislamu kwa michango wanayoendelea kuituo kwa ajili ya kituo hicho, na kuwaomba wazidishe ari katika kuichangia, ili iweze kurejea katika hali yake ya awali, ambapo zaidi ya shilingi milioni 80 zinahitajika kwa ajili ya kuzijenga upya studio hizo.
 
Mapema akizungumza kabla ya kukabidhi Kompyuta hizo, Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Mhe. Maalim Seif Sharif Hamad, amezidi kukitakia kheri kituo hicho ili kiweze kutoa huduma kama kawaida.
 
Amesema bado Radio hiyo itabakia kuwa na umuhimu wa kipekee katika kutoa taaluma mbali mbali zikiwemo zile zinazohusiana na  maadili ya kiislamu, jambo ambalo pia linaisaidia serikali katika kurejesha maadili mema kwa jamii.