Dodoma.
Spika wa Bunge, Anne Makinda amesema muda wa Bunge utaongezwa ili kutoa nafasi kwa serikali kuwasilisha Muswada wa Marekebisho ya Sheria ya Kodi ya Mapato (VAT).
Wiki iliyopita, Mbunge wa Mwibara, Kangi Lugola aliomba mwongozo na alipopewa nafasi alimlalamikia Spika wa Bunge kuwa katika ratiba ya bunge, haoni mahali ambapo kuna nafasi ya wabunge kujadili Muswada wa Marekebisho ya Sheria ya VAT.
Lugola, (CCM) baada ya kauli yake, alitishia kukusanya saini za wabunge kumwondoa Spika Makinda iwapo muswada huo hautaletwa katika Bunge la Bajeti na zaidi ni kwa ajili ya kufuta misamaha ya kodi isiyo na tija.
Muda mfupi baada ya kupitishwa kwa bajeti ya Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa mwaka wa fedha 2014/2015, Makinda alitangaza hatua hiyo ya Bunge kuongeza muda.
“Kwa mujibu wa kanuni zetu hatuingizi kitu kingine katika Bunge la Bajeti zaidi ya bajeti, lakini tunaangalia uwezekano wa kuongeza muda baada ya bajeti kwa siku chache kwa sababu ya mambo yanayotakiwa kufanyika,” alisema na kuongeza;
“Naambiwa kuwa Serikali inataka kuleta sheria inayohusiana na VAT.”
Makinda aliwataka wabunge kusoma vizuri kanuni za Bunge kwa sababu Spika hahusiki kuletwa muswada bungeni.
Katika hoja yake, mbunge huyo wa Mwibara, alisema nchi inapoteza Sh1.5 trilioni kwa misamaha ya kodi wakati bajeti ya Serikali kwa mwaka jana ina upungufu wa kiasi hicho hicho cha fedha.
“Kama hawajaleta muswada kiofisi, mimi siwezi kufanya chochote lakini nimesikia kuwa serikali inataka kuleta muswada huo,”alisema Makinda.
Makinda alisema kuwa kuongezwa kwa siku hizo kunalenga kuwawezesha wabunge kujadili ripoti ya migogoro ya ardhi nchini.
Alisema Kamati ya Bunge iliyopewa kuchunguza migogoro hiyo ilikwenda mbali zaidi na kuona vitu vingi ikiwemo matatizo yaliyopo katika mfumo.
0 Comments