MAHAKAMA nchini Sudan imemhukumu kifo mwanamke mmoja anayedaiwa kubadili dini yake na kuolewa na mwanamume mkristo.
Daktari Mariam Yahya Ibrahim Ishag, ambaye babake ni muislamu alishitakiwa kwa kosa la kuasi dini pamoja na kufanya zinaa kwa kuolewa na mwanamume mkristo, kitu ambacho dini ya kiisilamu imeharamisha kwa wanawake.
Mariam mwenye umri wa miaka 27 ambaye ni mjamzito pia atapata adhabu ya mijeledi 100 kwa kosa la zinaa. Maofisa wakuu wanasema kuwa icha ya Mariam kulelewa kwa njia ya kikristo yeye bado ni muislamu kwa sababu hiyo ndiyo dini ya babake.
Kwa kawaida wanawake waisilamu hawaruhusiwi kuolewa na wanaume wakristo ingawa wanaume waisilamu wanaruhusiwa kuwaoa wanawake wakristo.
Shirika la kimataifa la kutetea haki za binadamu Amnesty International linasema kuwa Bi. Ishag alilelewa kama mkristo muorthodoxi kwa sababu babake hakuwepo naye maishani mwake.
(HABARI: BBC SWAHILI)