Dodoma.
Serikali imekamilisha taratibu za ununuzi wa vichwa vipya 13 vya treni na mabehewa 355 ambayo yataanza kuwasili nchini kati ya Julai na Desemba mwaka huu.
Serikali inashirikiana na Serikali za Rwanda na Burundi katika uendelezaji wa mradi wa ujenzi wa Reli ya Dar es Salaam-Isaka-Musongati kwa kiwango cha kimataifa.
Waziri wa Uchukuzi, Dk Harrison Mwakyembe alitoa kauli hiyo bungeni mjini Dodoma juzi usiku wakati akiwasilisha bajeti ya wizara yake kwa mwaka wa fedha wa 2014/15 inayofikia Sh527 bilioni.
Alisema kazi inayoendelea sasa ni kumtafuta mshauri (Transact Advisor) atakayekuwa na jukumu la kuandaa, kusimamia na kuongoza mpango wa kuwapata wawekezaji watakaojenga reli hiyo.
“Kazi ya usanifu wa kina wa kuinua kiwango cha Reli ya Isaka-Mwanza ilianza Septemba 2013 na inatarajiwa kukamilika Julai 2014 kwa gharama ya Sh4.53 bilioni...Hatua hizi ni muhimu katika kutekeleza dhamira ya Serikali ya kuboresha Reli ya Kati kwa kiwango cha kimataifa (standard gauge)” alisema Dk Mwakyembe katika hotuba yake hiyo.”
Pia Dk Mwakyembe alisema kuwa tayari mtaalamu mwelekezi amepatikana kwa ajili ya kufanya upembuzi yakinifu na usanifu wa awali wa ujenzi wa Reli ya Mtwara-Songea-Mbambay.
Mkataba wa kutekeleza kazi hiyo itakayohusisha pia ujenzi wa reli ya mchepuko kwenda Mchuchuma na Liganga utasainiwa wakati wowote kabla ya mwisho wa Juni mwaka huu.
Pia mshauri mwelekezi, Kampuni ya Cowi kutoka Denmark ameanza kazi ya usanifu wa uboreshaji wa njia ya Reli ya Tanga-Arusha na usanifu huo utagharimu Sh5 bilioni.
Katika hatua nyingine, Dk Mwakyembe alisema Kampuni ya H.P Gauf ya Ujerumani inaendelea na kazi ya upembuzi yakinifu na usanifu wa awali wa ujenzi wa reli mpya ya Arusha-Musoma.
Ununuzi wa mabehewa
Dk Mwakyembe alisema katika mwaka ujao wa fedha wa 2014/2015, Serikali imetenga Sh126.9 bilioni kununua vichwa vipya 11 vya treni na mabehewa 204.
Alisema fedha hizo zitatumika pia kufanya matengenezo ya njia ya reli ya kati yenye mtandao wa urefu wa kilometa 2,707.Kwa mujibu wa Dk Mwakyembe, mkataba wa ununuzi wa vichwa vipya vya treni 13 ulisainiwa Aprili 2013 na vitaanza kuwasili nchini Desemba.
Pia alisema mkataba wa ununuzi wa mabehewa mapya 22 ya abiria ulisainiwa Machi 2013 na yanatarajiwa kuwasili Septemba.
Malipo kwa ajili ya vichwa hivyo vipya 13 na mabehewa hayo mapya 22 ya abiria yamekwishafanyika.
Dk Mwakyembe alisema mkataba mwingine wa ununuzi wa mabehewa 274 ya mizigo ulisainiwa Machi mwaka jana na yataanza kuwasili nchini Septemba mwaka huu.
“Malipo ya awali yalikamilika Februari 2014 na ya mwisho yanatarajiwa kukamilika kabla ya mwisho wa Juni mwaka huu,” alisema Waziri Mwakyembe.
Alisema ununuzi wa mabehewa 34 ya breki ulisainiwa Machi 2013 na malipo yote yalikamilisha na yataanza kuwasili nchini Julai mwaka huu.
Dk Mwakyembe alisema ununuzi wa mabehewa 25 ya kubebea kokoto yamenunuliwa na yanatarajiwa kuwasili nchini Julai mwaka huu.
Kwa mujibu wa Dk Mwakyembe katika kutekeleza miradi ya reli chini ya matokeo makubwa sasa (BRN), wizara yake iliidhinishiwa Sh165.6 bilioni kwa mwaka 2013/14.
“Hadi kufikia Aprili 2014 wizara yangu ilikuwa imepokea Sh145 bilioni sawa na asilimia 88 ya bajeti iliyoidhinishwa kwa ajili ya miradi yote ya maendeleo,” alisema.
Alisema kwa mwaka ujao wa fedha wa 2014/15, Serikali imetenga Sh129.9 bilioni kwa ajili ya kuunda upya vichwa vingine vya treni nane.
Dk Mwakyembe alisema fedha hizo zitatumika pia kununua mabehewa mapya ya mizigo 204 na kununua vichwa vipya vya treni 11.
Katika hatua nyingine, wizara hiyo imepanga kununua rada mbili za kuongoza ndege za kiraia zitakazogharimu Sh11.14 bilioni katika mwaka ujao wa fedha wa 2014/15.Dk Mwakyembe alisema wizara yake imeanza mazungumzo na Shirika la Kimataifa la Usafiri wa Anga (Iciao) ili kuweza kupata rada hizo kutoka kwa watengenezaji.
Waziri huyo alisema Mamlaka ya Usafiri wa Anga nchini imeanza kutumia mitambo ya satelaiti (ADS-B) ili kuimarisha usafiri wa anga wakati wa uongozaji wa ndege.
Mamlaka hiyo ilisaini mkataba na Kampuni ya Ujerumani ya Comsoft GmbH ili kuendelea na ufungaji wa satelaiti hizo katika nusu ya nchi upande wa Mashariki hadi juu ya Bahari ya Hindi.
“Awamu ya kwanza ya ufungaji wa satelaiti hizi itakayogharimu Sh1.99 bilioni unatarajiwa kukamilika Novemba, 2014,” alisema Waziri Mwakyembe.
Dk Mwakyembe alisema zabuni kwa ajili ya kufunga awamu ya pili itakayohusu eneo la nchi lililobaki ilifunguliwa Aprili mwaka huu na kazi ya uchambuzi wa zabuni hizo inaendelea.
0 Comments