Viongozi wa Afrika wanaokutana mjini Paris Ufaransa wamekubaliana kutangaza vita dhidi ya kundi la wapiganaji wa kiisilamu la Boko Haram.
Rais wa Ufaransa, Francois Hollande ambaye ni mwenyeji wa mkutano huo, amesema kuwa mataifa ya kikanda yameahidi kushirikiana na kuarifiana taarifa za kijasusi kuhusu kundi hilo ili kupambana nalo.
|
Mwezi jana kundi hilo liliwateka nyara zaidi ya wasichana miambili Kaskazini Mashariki mwa Nigeria ambako kundi hilo linaendeshea harakati zake.
Inaarifiwa kuwa kundi hilo lilifanya mashambulizi mapya usiku kucha nchini Nigeria na Cameroon.Maelfu ya watu wameuawa na wengine kuachwa bila makao kutokana na vita ambavyo vimekuwa vikiendeshwa na Boko Haram katika miaka ya hivi karibuni.
Mkutano uliofanyika mjini Paris, ulihudhuriwa na mwenyeji Rais Francois Hollande, Rais wa Nigeria Goodluck Jonathan, na marais wenzao kutoka Benin, Cameroon, Niger na Chad.
Baada ya mkutano huo bwana Hollande alisema washiriki wa mkutano huo, wamefikia mwafaka wa kimataifa na mkakati wa kikanda kupambana na kundi hilo.
Alisema kuwa mkakati huo utahusisha kushirikiana kijasusi , uchunguzi wa mipakani na kuwepo kwa vikosi vya nchi hizo katika maeneo ya mipakani na katika eneo linalozingira ziwa Chad pamoja na kutafuta uwezo wa kukabiliana na mashambulizi yanayofanywa na wapiganaji hao.
|
0 Comments