Rais jana aliziagiza Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii na ile ya Fedha kushirikiana Bohari Kuu ya Dawa (MSD) kuchukua hatua za dharura kupambana nao kwa kuhakikisha vinapatikana vipimo vya kutosha na dawa.PICHA|MAKTABA 
Dar/Arusha. 
Wakati raia tisa wa China wakibainika kuugua ugonjwa wa dengue na kulazwa hapa nchini, Rais Jakaya Kikwete amevunja ukimya na kuagiza wizara zake mbili kukabiliana na ugonjwa huo kwa dharura.
Ugonjwa huo uliingia nchini tangu mwaka 2010 lakini mlipuko wake mkubwa ulibainika Machi mwaka huu na hadi jana wagonjwa zaidi ya 400 walikuwa wameambukizwa, huku watatu wakiripotiwa kufariki dunia, akiwamo Daktari Bingwa wa magonjwa ya akili, Dk Gilbert Buberwa anayezikwa leo, Dar es Salaam.
Rais jana aliziagiza Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii na ile ya Fedha kushirikiana Bohari Kuu ya Dawa (MSD) kuchukua hatua za dharura kupambana nao kwa kuhakikisha vinapatikana vipimo vya kutosha na dawa.
Wachina walazwa
Taarifa kutoka Hospitali ya Aga Khan, Dar es Salaam zilieleza kuwa wagonjwa waliobainika kuugua homa hiyo hadi jana ni raia hao wa China na Watanzania wachache wenye historia ya kusafiri nje ya nchi hasa China, Ufilipino na Kusini mwa India.
Muuguzi katika kitengo cha magonjwa ya kuambukiza cha Aga Khan, Nyangee Lugoe alisema hospitali hiyo ilianza kupokea wagonjwa tangu Machi mwaka huu na kuanzia Aprili, raia wengi wa China wamegundulika kuwa na homa hiyo, ingawa baadhi walitibiwa na kuruhusiwa.
Agizo la Rais Kikwete
Akizungumza katika maadhimisho ya Siku ya Wauguzi Duniani huko Arusha, Rais Kikwete alisema: “Hili ni jambo la dharura la kitaifa lazima hatua muafaka zichukuliwe kudhibiti ugonjwa huu, ambao asili yake ni nchi za Asia na Bara la Amerika.”
Alisema dalili za ugonjwa huo ambao unasababishwa na mbu aina ya Aedes Egyptie anayeuma mchana ni homa kali ya kuumwa kichwa, maumivu ya viungo na kutoka damu puani na kwenye fizi na kupoteza fahamu.
“Napenda kutoa wito mtu yoyote ambaye atapata dalili za ugonjwa huu, aende mara moja hospitalini ili afanyiwe vipimo badala ya kunywa dawa,” alisema.
Tayari Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii imetangaza kuanza kuchukua hatua za dharura kukabiliana na ugonjwa huo, ikiwa ni pamoja na uelimishaji na uhamasishaji wa jamii kuchukua tahadhari.
Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Charles Pallangyo alisema jana kuwa wizara yake imetoa hadhari ya ugonjwa huo kupitia kwa waganga wakuu wa mikoa na wilaya kote nchini na itatoa mafunzo maalumu kwa watumishi wa afya ikiwajumuisha madaktari na mafundi maabara ili kuwajengea uwezo.Aidha, wizara hiyo itaanzisha vituo maalumu vya ufuatiliaji wa ugonjwa huo katika hospitali za Mwananyamala, Amana na Temeke.
Ugonjwa kutoka nje
Daktari Kiongozi na Mtaalamu wa Homa ya dengue katika Hospitali ya Mwananyamala, Dk Mrisho Lupinda alisema upo uwezekano mkubwa kuwa virusi hivyo viliingia nchini kutokana na mwingiliano na urahisi wa watu kusafiri kati ya Tanzania na nchi za Mashariki ya Mbali.
“Namna watu wanavyopata nafasi ya kusafiri kwa haraka kwenda sehemu moja na kurudi kwa shughuli mbalimbali ikiwamo biashara ndivyo namna maambukizi yanavyoenea kwa urahisi. Hii inawezekana kabisa kwamba mwingiliano wa kibiashara umechangia kwa kiasi fulani,” alisema.
Alisema ugonjwa huo ni wa kawaida katika maeneo ya kitropiki kwenye mabara yote, lakini umezoeleka zaidi kwenye nchi za Mashariki ya Mbali hasa bara la Asia.
Alisema mbu wanaoambukiza ugonjwa huo walikuwapo nchini kwa zaidi ya miaka 300 iliyopita lakini hawakuwa na virusi hivyo.
Hakuna unyanyapaa
Mkurugenzi wa Tiba katika Hospitali ya Aga Khan, Dk Jaffer Dharsee alisema licha ya ugonjwa huo unaua na kuambukiza, wananchi hawapaswi kuwa na unyanyapaa kwa waliogua.
“Baada ya taarifa kuenea kwa kasi, kuna watu wameogopa na wanadhani wale waliopata hawapaswi kuguswa au kusogelewa lakini huu ni ugonjwa usioambukizwa kwa njia hizo kama ukoma,” alisema.
Alisema mgonjwa wa dengue anahitaji tiba ya dalili zinazojitokeza na ili asiambukize atahitaji kulala kwenye chandarua hata kama ni mchana,” alisema.