Rais Jakaya Kikwete. Picha na Maktaba
Dodoma na Dar.
Rais Jakaya Kikwete anatarajiwa kuwasili Dodoma keshokutwa, ikiwa ni siku moja kabla ya kuwasilishwa kwa Bajeti Kuu ya Serikali kwa mwaka wa fedha 2014/15.
Habari zilizopatikana jana zinasema Rais ataongoza kikao cha Baraza la Mawaziri kitakachopewa muhtasari kuhusu Bajeti ya Serikali ya mwaka ujao wa fedha na baadaye atafuatilia uwasilishaji wa bajeti hiyo bungeni akiwa Dodoma.
Mkurugenzi wa Mawasiliano Ikulu, Salva Rweyemamu alisema asingeweza kuzungumzia suala hilo kwa kuwa yuko likizo lakini akaweka bayana kwamba kwa kawaida kabla ya bajeti kuwasilishwa bungeni, lazima Baraza la Mawaziri lipewe muhtasari wa bajeti husika.
“Ni kawaida kabla ya bajeti kuwasilishwa, Rais huongoza kikao cha Baraza la Mawaziri yaani pre budget cabinet meeting ambako Waziri wa Fedha hutoa briefing (muhtasari) kuhusu maeneo muhimu ya bajeti, kwa hiyo siyo jambo jipya ni suala la kawaida,” alisema Rweyemamu.
Itakumbukwa kuwa mwaka jana kabla ya kusomwa kwa bajeti ya 2013/14, Rais Kikwete alikuwa Dodoma ambako pamoja na kukutana na mawaziri, pia alifanya kikao na Kamati ya Bunge ya Bajeti.
Hata hivyo, uwepo wake mjini Dodoma safari hii umekuja wakati kukiwa na dalili za mvutano mkubwa kati ya Bunge na Serikali kutokana na kutotolewa kwa fedha za kutosha za maendeleo kwa mwaka wa fedha unaoisha Juni 30 mwaka huu.
Taarifa zinasema bajeti inayomalizika mwishoni mwa mwaka huu, inapungukiwa kiasi cha Sh1.8 trilioni, huku Serikali ikilaumiwa na wabunge kwa kutoa misamaha ya kodi inayofikia Sh1.52 trilioni, ambayo ingepunguza nakisi iliyopo kwenye bajeti kwa asilimia 84.4.
Wakati wa mjadala wa bajeti za wizara tangu kuanza kwa Bunge la Bajeti Mei 6 mwaka huu, wabunge wamesikika mara kadhaa wakilalamika kwamba fedha za maendeleo zilizotolewa kwa wizara katika bajeti ya 2013/14 ni kati ya asilimia 25 na 30, jambo ambalo limesababisha kukwama kwa miradi mingi.
Keshokutwa itakuwa siku ya mwisho ya mashauriano baina ya Serikali kupitia Wizara ya Fedha na Bunge kupitia Kamati yake ya Bajeti inayoongozwa na Mbunge wa Bariadi Magharibi, Andrew Chenge.
Mazungumzo hayo yaliyoanza Juni 5 mwaka huu, yalilenga kuangalia uwezekano wa kutafuta vyanzo vipya vya mapato ili kuwezesha kuzingatiwa kwa ushauri wa wabunge, pamoja na kusaka fedha kuziba pengo la Sh1.8 trilioni katika bajeti ya 2013/14.
Alipoulizwa jana, Chenge hakuwa tayari kuzungumzia hatua iliyofikiwa katika mashauriano hayo na badala yake alisema kwa ufupi: “Ndugu yangu mambo ya Bunge, tutakutana kwenye taarifa yetu ya kamati tutakayoiwasilisha bungeni.” Kamati ya Bajeti katika maoni yake iliyoyatoa Juni 17 mwaka jana kuhusu Bajeti ya Serikali ya 2013/14, iliweka bayana kuwapo kwa udhaifu mkubwa katika ukusanyaji wa mapato, baadhi ya wizara kutumia fedha nyingi kuliko ilivyoidhinishwa na Bunge na Serikali kuwa na matumizi makubwa kuliko mapato yake.
Sehemu ya taarifa hiyo iliyosomwa na Chenge ilibaini kuwa katika bajeti ya 2011/12 Serikali ilitumia kiasi cha Sh1.3 trilioni ya mapato yake na mwaka wa fedha uliofuata 2012/13 ilizidisha kiasi cha Sh1.5 trilioni.“Hali hii imesababisha Serikali kuendelea kukopa kutoka nje na ndani kwa ajili ya kufidia pengo la upungufu wa fedha. Kamati imebaini kuwa kuendelea kukopa ambako hakuendi sambamba na juhudi za ukusanyaji wa mapato, kutaendelea kuwa mzigo kwa nchi kwani itaendelea kukopa na kuongeza kiasi cha matumizi,” inasomea sehemu ya taarifa hiyo.
Habari zilizopatikana kutoka Dodoma zinasema vikao vya majadiliano baina ya Serikali na Bunge vinaendelea leo baada ya kusitishwa Jumamosi saa tano usiku, huku kukiwa na mjadala mkali kuhusu uwezekano wa kupatikana kwa fedha za kutekeleza bajeti inayofikia ukomo wake mwezi huu.
“Kwa kweli mvutano umekuwa mkali kati ya Waziri wa Fedha na watendaji wa wizara hiyo kwa upande mmoja, dhidi ya wajumbe wa Kamati ya Bajeti kwa upande mwingine. Kubwa ni kutizama vyanzo vipya vya mapato,” kilidokeza chanzo chetu.
Habari zinasema katika kikao kilichofanyika Ijumaa, hoja iliyotawala ilikuwa ni kutafutwa kwa vyanzo mbadala vya mapato na wajumbe wa kamati hiyo waliibana Serikali wakiitaka iondokane na utamaduni wa kutoza fedha kutoka kwenye soda, bia, maji na sigara pekee.
Hata hivyo, wiki iliyopita Spika wa Bunge, Anne Makinda alisema katika kikao hicho cha Kamati ya Bajeti na Serikali hakuna fedha zitakazoongezwa na kitakachofanyika ni kutoa fedha kutoka eneo moja na kupeleka eneo jingine lenye umuhimu na uharaka katika utekelezaji wake.
Miongoni mwa maeneo ambayo wabunge wanaitaka Serikali kuongeza fedha ni sekta ya maji ambayo inapendekezewa iundiwe mfuko wa maji vijijini ili kuikabili kero hiyo ambayo imekuwa na athari kubwa kwa wananchi.
Shinikizo la wabunge kuhusu suala la mfuko wa maji limekuja wakati Wizara ya Maji hadi sasa ikiwa inahitaji kupewa kiasi cha Sh126 bilioni ambazo ziliidhinishwa katika bajeti ya 2013/14.
Katika kujaribu kupunguza nakisi hiyo, Serikali ilikubali kutafuta kiasi cha Sh100 bilioni kabla ya mwaka huu wa fedha kumalizika ili zielekezwe katika miradi ya maji na taarifa zinasema tayari imetoa Sh80 bilioni.
Wakati wa mjadala wa Wizara ya Afya, wabunge pia walichachamaa wakikosoa hatua ya kupunguzwa kwa kiasi cha Sh131 bilioni ikilinganishwa na mwaka wa fedha unaomalizika na kwamba punguzo hilo litaathiri kwa kiasi kikubwa tiba na huduma za afya nchini.
Mwaka ujao wa fedha, wizara hiyo imeidhinishiwa Sh622 bilioni, ikilinganishwa na kiasi cha Sh753 bilioni zilizoidhinishwa 2013/14.
Wizara ya Uchukuzi nayo ilikuwa na wakati mgumu wakati wa mjadala wa makadirio yake ya matumizi, pale wabunge walipochachamaa wakitaka fedha ziongezwe kwa ajili ya Shirika la Ndege (ATCL), ukarabati wa meli ya MV Victoria na upanuzi wa Uwanja wa Ndege wa Mwanza.
|
0 Comments