Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Ukanda wa Uwekezaji (EPZA), Adelhelm Meru (kulia) akisalimiana na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Watu wa China, Dk Li Yuanchao wakati alipotembelea Kiwanda cha Nguo cha Tooku kilichopo ndani ya mamlaka hiyo Mabibo External jijini Dar es Salaam juzi . Katikati ni Waziri wa Viwanda na Biashara, Dk Abdallah Kigoda. Picha na Silvan Kiwale
Dar es Salaam.
Wawekezaji kutoka nchini China wameshawishiwa kuwekeza katika maeneo ya Mamlaka ya Ukanda Maalumu wa Uwekezaji nchini (EPZA) yaliyotengwa kwa ajili hiyo katika mikoa mbalimbali nchini.
Rai hiyo ilitolewa na Mkurugenzi Mkuu wa EPZA, Dk Adelhelm Meru, hivi karibuni jijini Dar es Salaam, alipokuwa akitoa mada kuhusu maeneo maalumu ya uwekezaji Tanzania na mamlaka yake wakati wa kongamano la pili la biashara kati ya Tanzania na China.
“Serikali tayari imetenga hekta 22,000 katika eneo la uwekezaji Bagamoyo, hivyo tunawakaribisha muwekeze katika maeneo hayo huru ya uwekezaji Tanzania. Tunataka eneo hili kuwa la viwanda na kituo cha biashara,” alisema Meru.
Tayari China imesajili miradi 522 TIC yenye thamani ya Dola za Marekani 2.4 bilioni inayotarajiwa kuzalisha ajira 77,335.
Dk Meru alisema Serikali kwa kushirikiana na sekta binafsi iko mbioni kuendeleza miundombinu katika eneo hilo na kwamba ni wakati mwafaka sasa kwa wawekezaji kuja na kutekeleza azma yao.
Alisema kuwa bandari kubwa nchini, itajengwa katika eneo hilo na kuwa itabadilisha kwa kiwango kikubwa mwonekano wa Bagamoyo, pamoja na kuwapo mpango wa kujenga kiwanja cha ndege cha kisasa na reli itakayounganishwa na ile ya Kati na Tazara.
Kwa mujibu wa mkurugenzi huyo, EPZA imetenga maeneo huru na maalumu ya uwekezaji katika mikoa 20 yakiwa na ukubwa wa ekari 500-9,000 kila moja.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Maendeleo ya Viwanda wa Muungano wa Wafanyabiashara, Viwanda na Kilimo (TCCIA), Adam Zuku alisema kuwa Watanzania wanatakiwa kuzidisha ujuzi na taaluma ili kuweza kushirikiana kati ya nchi hizo mbili.
Hivi karibuni, EPZA ilisaini makubaliano na Benki ya Maendeleo Tanzania (TIB) kwa ajili ya kupata mikopo ya kujenga miundombinu itakayovutia wawekezaji kuanzisha viwanda katika maeneo yake maalumu.
Kongamano hilo lilishirikisha kampuni zaidi ya 100 kutoka China na kampuni zaidi ya 120 za Kitanzania.
|
0 Comments