Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF), Seif Sharif Hamad (Maalim Seif).PICHA|MAKTABA
Dar es Salaam.
Wakati Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF), Seif Sharif Hamad (Maalim Seif) akiwa mgombea pekee wa nafasi ya katibu mkuu wa chama hicho, makada wawili wamejitokeza kumvaa Profesa Lipumba katika nafasi ya uenyekiti.
Maalim Seif ambaye ni Makamu wa Kwanza wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa Zanzibar, ameshikilia nafasi hiyo ya ukatibu mkuu wa CUF kwa miaka 15 tangu mwaka 1999 alipoachana na cheo cha umakamu mwenyekiti, na iwapo atapitishwa na mkutano huo atakuwa amekalia cheo hicho kwa miaka 20 mfululizo.
Akitoa taarifa kuhusiana na mkutano mkuu wa sita wa chama hicho unaotarajia kuanza leo Dar es Salaam, Mkurugenzi Haki za Binadamu, Habari na Uenezi, Salum Biman alisema hakuna mwanachama aliyejitokeza kupambana na Maalim Seif.
“Hiyo nafasi ilitangazwa mwezi mzima, lakini hakuna mwanachama aliyejitokeza,” alisema na kuongeza;“Hata wewe ungekuwa mwanachama wa CUF, ungekuwa na haki ya kugombea nafasi hiyo, hakuna mwanachama aliyekatazwa.”
Kuhusu nafasi ya mwenyekiti, Biman alisema kuna wanachama wawili wamejitokeza kupambana na Profesa Lipumba. Aliwataja wagombea waliojitokeza kuwa ni Chief Lutayosa Yemba kutoka Shinyanga na mwingine aliyemtaja kwa jina la Ibrahim kutoka Mkoa wa Pwani. Hata hivyo, taarifa nyingine zimemtaja pia Mbezi Adam Bakar kutoka Temeke, Dar es Salaam.
“Wagombea hao ndiyo watakaopambana na Profesa Lipumba katika nafasi ya uenyekiti,” alisema.
Kuhusu nafasi ya Makamu Mwenyekiti, Bimani alisema aliyekuwa anashikilia nafasi hiyo, Machano Khamis ameachia ngazi na kumpisha Waziri wa Afya wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa ya Zanzibar, Juma Haji Duni.
Alisema mkutano huo utawashirikisha wajumbe 800 kutoka Tanzania Bara na Zanzibar na utafanyika kwa siku tano, unatarajia kumalizika Juni 27, mwaka huu.
“Taarifa mbalimbali za chama zitasomwa baada ya miaka mitano ya utendaji. Katika mkutano huo, mwenyekiti Profesa Lipumba na katibu mkuu wake wataachia ngazi ili kupisha uchaguzi mkuu uweze kufanyika.”
Aliongeza kuwa mkutano huo utateua pia wajumbe 45 wa Baraza Kuu kutoka kila kanda na wajumbe wanawake ambao ni asilimia 30 ya wajumbe wote wa mkutano mkuu.
“Hadi sasa Wilaya 10 za Zanzibar na 90 za Bara zimeshakamilisha uongozi wa wilaya, hivyo zitatuwezesha kufanikisha uchaguzi katika mkutano mkuu,” alisema.
Mbali na uchaguzi huo alisema mkutano huo utarekebisha baadhi ya vipengele vya katiba na kanuni za chama hicho.Alisema baada ya uchaguzi wa kamati kuu, mwenyekiti kwa kushirikiana na makamu watateua wakurugenzi wa idara ambao watathibitishwa na Baraza Kuu kabla ya kupendekeza majina ya manaibu katibu ambao watathibitishwa na uongozi.
|
0 Comments