majeshi ya marekani Iraq
Marekani imetangaza kuwa inatuma wanajeshi 275 nchini Iraq kusaidia kulinda maafisa na Ubalozi wake mjini Bagdad.
Tangazo hilo limetolewa wakati maafisa wa Marekani na Iran wakifanya mazungumzo kuhusu hali nchini Iraq katika kongamano linalojadili maswala ya nyuklia mjini Viena.
Rais Obama ameandika barua kwa baraza la Congress kueleza mipango ya kutuma wanajeshi hao 275 mjini Baghdad.

Anasema jukumu la kikosi hicho ambacho kitakabidhiwa silaha ni kulinda raia wa Marekani wanaoishi nchini Iraq na mali yao.
Wanajeshi hao wataendelea kukaa nchini humo hadi hali ya usalama itakapoimarika.

Matumaini yanadidimia

Hatahivyo hakuna ishara yoyote ya hali kuimarika huku kundi la wapiganaji la ISIS likiendeleza harakati zake katika baadhi ya maeneo ya Iraq.
Rais Obama ambaye anaonekana kutafakari kuhusu hatua ambazo Marekani inaweza kuchukua, anashauriwa na maafisa kutoka kitengo cha usalama wa kitaifa.
Kwingineko maafisa wa Marekani wamethibitisha kuwa wamefanya mazungumzo mafupi na maafisa kutoka Iran kuhusu hali nchini Iraq.
Awali waziri wa mambo ya nje wa Marekani John Kerry alisema yuko tayari kushauriana na Iran ambayo wakati mmoja ilikua hasimu wa Marekani. Hatahivyo maafisa wa Marekani wametupilia mbali uwezekano wa ushirikiano wa kijeshi kati ya nchi hizo.