Kamanda wa Jeshi la Polisi mkoa wa Singida, SACP Geofrey Kamwela.
Na Nathaniel Limu, Singida
JESHI la Polisi mkoa wa Singida limefanikiwa kukamata watu wawili kwa tuhuma ya kumiliki lita 23 za pombe haramu ya gongo na mitambo sita ya kutengenezea pombe hiyo haramu.
Kamanda wa Jeshi la Polisi mkoa wa Singida, SACP Geofrey Kamwela amesema Elitruda Omari (40) mkazi wa Karakana Singida mjini,amekamatwa akimiliki lita 15 za pombe haramu ya moshi na mitambo mitano ya kutengenezea pombe hiyo.
Amesema mtuhumiwa Elitruda alikamatwa mei 28 mwaka huu saa 5.55 usiku huko maeneo ya Karakana mjini Singida.
Katika tukio la pili,Kamwela amesema John Geofrey (51) mkulima na mkazi wa kijiji cha Ruruma kata ya Kiomboi tarafa ya Kisiriri wilaya ya Iramba,amekamatwa akimiliki lita nane za pombe haramu ya moshi na mtambo moja wa kutengenezea pombe hiyo.
Amesema John amekamatwa mei 28 mwaka huu saa 7.45 mchana huko katika kijiji cha Ruruma.
“Imeelezwa na rai wema kuwa John ni mtengenezaji na muuzaji maarufu wa pombe ya moshi katika kata hiyo ya Kiomboi”,amesema.
Kamanda Kamwela,amesema kuwa upelelezi ukikamilika,watuhumiwa hao watafikishwa mahakamani kujibu tuhuma inayowakabili ya kumiliki pombe haramu ya Gongo.