Stori: Shakoor Jongo na Musa Mateja
ZIKIWA zimepita wiki kadhaa tangu kuripotiwa kupatanishwa kwa mastaa wawili katika tasnia ya filamu Bongo, Wema Sepetu na Kajala Masanja, taarifa zisizo na shaka zilizotua kwenye meza ya Ijumaa Wikienda zinaeleza kwamba upatanisho huo haukusaidia chochote na sasa bifu jipya limeibuka kati yao.Kwa mujibu wa chanzo chetu cha ndani kilichoomba hifadhi ya jina lake, zoezi la upatanishi kati ya mastaa hao lililofanyika kwenye msiba wa dairekta wa filamu za Kibongo, George Tyson, Mbezi Beach jijini Dar lilikuwa sawa na kazi bure.
“Hakuna yeyote kati yao aliyekuwa na nia ya dhati ya kumaliza tofauti zilizokuwepo, walikubali kupatana kwa sababu ya heshima ya waliokuwa wanawapatanisha lakini kiukweli ilikuwa ni sawa na danganya toto, bifu limelipuka upya,” kilisema chanzo hicho ambacho ni rafiki wa karibu wa mastaa hao wakubwa mjini.
TEAM WEMA, TEAM KAJALA WANOGESHA BIFU Kwa mujibu wa sosi wetu, ukiachilia mbali kukosekana kwa utayari wa kupatanishwa kati ya wawili hao, pande mbili za mashabiki wao wenye ushawishi mkubwa kwenye mitandao ya kijamii waliojipachika majina ya Team Wema na Team Kajala, zimekuwa zikinogesha bifu hilo kwa kumwagia petroli kwenye moto, hali inayozidi kutibua mambo.“Sikia nikwambie, kuna vitu vinafanyika katika mitandao ya kijamii hasa Instagram kuhusiana na hizi pande mbili halafu wahusika wakuu wanajifanya hawazijui, kuna Team Wema ambayo inamsapoti Wema na ile ya Kajala inayoitwa Team Kajala, wenyewe wanawajua fika ni akina nani wanaounda pande hizo ila ukiwauliza wanajifanya hawajui chochote.
“Wengine wananunuliwa mpaka simu za kisasa zenye uwezo wa kufungua mitandao ya kijamii ili wasambaze uzushi na uongo kuhusu upande pinzani, sasa timu hizo ziliposikia juu ya upatanisho huo, ziliwajia juu wahusika ambapo kila mmoja kwa upande wake alikanusha kupatana na mwenzake,” kilizidi kutiririka chanzo hicho.KAJALA HATAKI KABISA SULUHU
Chanzo chetu kiliendelea kufunguka kuwa Kajala hataki kabisa kusikia kuhusu mambo ya suluhu kwa sababu Team Wema imemdhalilisha sana mtandaoni kiasi cha kumpa wakati mgumu kujieleza mbele ya mwanaye, Paula ambaye inadaiwa naye aliyashuhudia matusi hayo ya nguoni.
“Yaani Kajala anasema labda Wema mwenyewe ndiyo aende kumuomba radhi kwa kashfa zilizokuwa zinatolewa na timu yake anaweza kumfikiria mara mbilimbili kuhusu suluhu na siyo kusuluhishwa juujuu tu kama ilivyotokea,” alizidi kutiririka sosi wetu na kuongeza:
“We si unaona mara ngapi Wema na Kajala wanakutana sehemu na wewe mwenyewe kama mwandishi unashuhudia, umewahi kuwaona wakiwa pamoja au hata kusalimiana?”
MSIKIE KAJALA Baada ya kusikia kauli hizo kutoka kwa chanzo chetu, kama kawaida ya Ijumaa Wikienda liliingia mzigoni kutafuta mzani wa habari ambapo wa kwanza kutafutwa alikuwa ni Kajala ambaye hakutaka kabisa kulizungumzia kwa kina suala hilo. Hebu msikie:
“Kiukweli mi naona hili tatizo letu linachangiwa na hizi timu ambazo zipo kwa ajili ya kuongeza matatizo. Nasikia eti baada ya siku ile mimi na Wema kupatanishwa, watu wa timu yake walimpigia kumuuliza, akakataa kuwa hajakubali kupatanishwa na mimi ili kuwafurahisha watu wake, sasa unategemea mimi nitasema nini? Nafikiri siyo rahisi mimi kukaa karibu na Wema kama zamani,” alisema Kajala.
WEMA NAYE Kwa upande wa Wema yeye alishangaa habari hizo na kutoa dukuduku lake kwa kusema anachojua ni kwamba hana bifu na mtu yeyote, siyo Kajala tu bali mtu yeyote ambaye walikuwa na tofauti huko nyuma yeye hana bifu naye tena.
“Mi nadhani watu wanahitaji kuona picha ambayo tumepiga pamoja na Kajala ndiyo waamini kuwa tumemaliza bifu letu, unajua huu unaokuja ni Mwezi Mtukufu wa Ramadhan na mimi ni mtoto wa Kiislam sasa nitafungaje Ramadhan huku nikiwa na bifu na mtu?” alisema Wema. Kukinzana kwa maelezo ya wawili hao kunatosha kuonesha jinsi ambavyo suluhu ya awali haikuweza kumaliza bifu kati yao.
KUTOKA KWA MHARIRI Wema na Kajala nyie ni wasanii wakubwa ambao jamii inawatazama kama kioo chao. Haipendezi kuendeleza malumbano yasiyo na msingi, huu si wakati wa kuwekeana visasi bali sameheaneni kutoka ndani ya mioyo yenu na mshirikiane kuisimamisha sanaa ya filamu za Kibongo.
|
0 Comments