Waziri Mkuu, Mizengo Pinda.PICHA|MAKTABA
Songea. 
Waziri Mkuu, Mizengo Pinda amewataka Watanzania wasikubali kuchagua viongozi wanaotafuta uongozi kwa kutumia fedha kwani zinaweza kuleta machafuko.
Alisema hayo jana wakati wa ibada maalumu ya kumsimika Askofu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Dayosisi ya Ruvuma, Amon Mwenda kwenye kanisa hilo la Usharika wa Songea iliyohudhuriwa na mamia ya waumini na viongozi mbalimbali.
“Ndugu zangu ninawaambia kuwa msigeuze uchaguzi kuwa mtaji, bali tuzingatie taratibu na sheria za uchaguzi ambazo ndiyo mwongozo unaoweza kutusaidia.
“Ninawasihi wananchi wawe makini na viongozi wanaopenda kutoa rushwa hasa katika kipindi hiki cha kuelekea kwenye Uchaguzi Mkuu. Kama mtu ana nia ya kweli ya kuongoza ni kwa nini atumie fedha ili kupata nafasi ya uongozi?” alisema na kuongeza:
“Tatizo ni kwamba hata wananchi hivi sasa wanakubali kupokea kile kinachotolewa na wagombea. Atakuja huyu atakupa hiki na mwingine naye atakupa kile, lakini ujue akiingia madarakani anaanza kurudisha haraka vile alivyowagawia.”
Aliwaomba viongozi wa dini na waumini kuendelea kuliombea taifa ili Mungu aliepushe na janga la watu kupenda rushwa.
Alitumia fursa hiyo pia kuwaomba wazidi kuuombea mchakato wa kupata Katiba Mpya ili wajumbe wote warejee ndani ya Bunge na kuikamilisha kazi waliyoianza.
Alisema Watanzania kwa sasa hivi wanahitaji kumwomba Mungu ili waendelee kuwa na amani.
Waziri Mkuu pia aliwataka Watanzania kujikita zaidi katika kilimo ambacho kitaweza kuwakomboa na kuondoa umaskini unaowakabili.
Alisema kila mwananchi anapaswa kufanya kazi kwa bidii ili aweze kumudu maisha yake ya kila siku akitolea mfano wa shughuli za kilimo na ujasiriamali badala ya kusubiri kusaidiwa.
Waziri Pinda alisema Dayosisi mpya ya Ruvuma inapaswa kuweka mipango yakinifu ya maendeleo ambayo itaweza kuisaidia Serikali kupunguza changamoto zilizopo kwa kuanzisha miradi ya elimu, afya na shughuli mbalimbali za kijamii.
Awali, akitoa hotuba yake ya kwanza mara baada ya kusimikwa rasmi, Askofu Mwenda alisema dayosisi mpya ya Ruvuma imezaliwa katika kipindi chenye changamoto nyingi za kidunia na utandawazi ukiwamo mmomonyoko mkubwa wa maadili.Hata hivyo, akiainisha malengo ya dayosisi hiyo ambayo anakuwa Askofu wake wa kwanza, Askofu Mwenda alisema mbali ya kufundisha neno la Mungu, dayosisi hiyo itahimiza ufanyaji kazi ili wakazi wake wawe na akiba ya chakula cha kutosha.
Alisema watashirikiana na Serikali na wadau wa ndani na nje kutoa huduma za kijamii hasa elimu na afya.
Aliahidi kukabiliana na changamoto za sasa ambazo alizitaja kuwa ni mmomonyoko wa maadili, rushwa, mauaji ya albino, unajisi wa watoto na ubakaji wa wanawake.
Akitoa shukrani kwa niaba ya waumini wa kanisa hilo, Askofu Mkuu wa KKKT, Dk Alex Malasusa alisema Kanisa lingependa kupata viongozi ambao ni wacha Mungu.
Askofu Malasusa alisema inashangaza kuona kuna baadhi ya watu wanagombea nafasi za uongozi lakini hawana mapenzi na Mungu aliyewaumba watu anaotaka kuwaongoza.