Na Henry Kilasila, Iringa
Wahandisi wa Shirika la Umeme nchini (TANESCO) wanaonolewa katika kutambua nguzo bora za kusambazia umeme wameanza mafunzo ya vitendo ya ukaguzi na utambuzi wa nguzo bora na salama katika baadhi ya viwanda vya kuzalishia nguzo hizo mkoani Iringa.
Ziara ya wahandisi hao wa TANESCO inalenga katika kuwawezesha katika kukabiliana na matumizi ya nguzo zisizo na ubora na ili kuongeza ufanisi na usalama katika zoezi la kusambaza umeme nchini.
Wahandisi hao wamepata fursa ya kutembela kiwanda cha Sao Hill kilichopo Mafinga mjini Iringa ikiwa ni mafunzo kwa vitendo juu ya utambuzi wa nguzo bora.
Washiriki waliweza kuona namna uzalishaji na utayarishaji wa nguzo unavyofanyka ikiwa ni pamoja na ukaguzi wa nguzo kabla haijawekewa dawa na ukaguzi wa nguzo baada ya kuwa ya kuwekewa dawa.
Akivitaja vitu vinavyoangaliwa kabla nguzo haijawekewa dawa Bw. Emmanuel Simkoko ambae ni mkaguzi kutoka Kampuni ya Ukaguzi wa Ubora ya SGS ya jijini Dar es Salaam, alisema vitu vya kuzingatia katika zoezi la utambuzi wa ubora wa nguzo ni pamoja na aina ya mti unaotumika katika kuandaa nguzo hizo, ukubwa, pamoja na kimo cha nguzo husika.
“Kuna vitu vya kuzingatia wakati wa kuchambua aina ya ubora wa nguzo, ni muhimu kujua aina ya mti ili kubaini hali ya unyevunyevu, na masuala mengine ya utaalamu ikiwamo vipimo vya nguzo husika,” alisema Bw. Simkoko.
Kwa mujibu wa Bw. Simkoko, nguzo bora haitakiwi kuwa na hali ya unyevunyevu kuvuka 25%, pamoja na ukubwa wa kitako cha nguzo kisipungue milimita 20 na juu ya nguzo isipungue milimita 20.
Wahandisi hao walielimishwa sifa nyingine ya nguzo bora kuwa ni pamoja na kuangalia nguzo kama imeliwa na wadudu, umbo la nguzo iliyo panda haifai kwa kuwa haitoweza kukidhi kazi husika.Bw. Simkoko alihitimisha kwa kuwaelimisha wahandisi hao namna ya kuwekea dawa nguzo zilizo bora, “Baada ya nguzo kuwekewa dawa huwafanyiwa majaribio kuangalia dawa kama imewekwa ipasavyo, na tuna utaratibu wa kuzifanyia majaribio kila mwezi,” aliongeza Bw. Simkoko.
Wahandisi wa TANESCO wapo mkoani Iringa kwa mafunzo ya wiki mbili yenye lengo la kuwawezesha wataalamu hao kuwa na weledi wa hali ya juu katika kutambua nguzo zenye sifa na umadhubuti na salama katika zoezi la usambazaji umeme nchini.
CAPTIONS
Ukaguzi 1
Mhandisi Donart Makingi (Kushoto) kwa niaba ya Meneja wa Usalama kazini akitoa maelekezo kwa wahandisi namna ya kuzingatia usalama katika eneo la kazi ikiwa ni pamoja na kuto kupanda kwenye nguzo, ama kugusa vifaa vya kazi bila kupata muongozo.
Ukaguzi 2 – 4
Wahandisi wa Shirika la Umeme Nchini (TANESCO) wakiwa katika mazoezi mbalimbali ya kubaini nguzo borayanayofanyika katika Kiwanda cha Sao Hill, mkoani Iringa.
Ukaguzi 5
Bw. John Mwaura Njenga ambae ni Meneja wa Poles and Timber Implementation akitoa maelezo kwa Wahandisi wa TANESCO namna kiwanda kinavyofanya kazi.
Ukaguzi 6
Wahandisi wakiwa maabara wakifanya majaribio ya namna kiasi cha dawa kilivyoingia ndani ya nguzo wakipata na maelekezo kutoka kwa Boniface Mwansatu ambae ni Mdhibiti Ubora kutoka Kampuni ya SGS.
Ukaguzi 7
Wahandisi wa TANESCO wakifuatilia maelekezo ya namna mtambo wa kuwekea nguzo dawa inavyofanya kazi katika kiwanda cha Sao Hill.
Picha zote na Henry Kilasila.
0 Comments