Stori: Dustan Shekidele,Morogoro
Mfalme wa Rhymes Bongo, Seleman Msindi ‘Afande Sele’ ameshindwa kustahimili msiba wa mkewe, Asha Msindi (34) na kujikuta akizimia msibani wakati wa maziko, Risasi Jumamosi lina stori ya kusikitisha.Tukio hilo ambalo liliibua simanzi nzito mkoani hapa na kuweka historia lilijiri juzi, Alhamisi katika Mtaa wa Amani, Mji Mkuu, alipokuwa akiishi Asha na mama yake.“Alipigiwa simu na baadhi ya ndugu wa mke kumueleza habari za msiba, hakushtuka sana maana hakuwa ameamini moja kwa moja hivyo akasema ataamini atakapofika msibani na kukuta msiba,” alisema mtu huyo wa karibu ambaye aliomba hifadhi ya jina gazeti.AZIMIA
Mtu huyo wa karibu alizidi kueleza kuwa, mara baada ya kufika nyumbani hapo na kukuta ndugu, jamaa na marafiki wamekusanyika ndipo Afande alipoanguka na kuzimia kwa takriban saa nne kisha akaziduka.
“Alipofika pale nyumbani kwa mkewe na kukuta umati ukiwa msibani, alijitahidi akaingia ndani na alipomuona mama mkwe wake, hapohapo alianguka na  kuzimia,” alisema mtu huyo.APEPEWA
Rafiki huyo wa Afande alizidi kueleza kwamba, baada ya kuzimia, ndugu wa mke walimlaza kwenye kochi kisha baadaye rafiki zake walimchukua na kumpeleka nyumbani kwake maeneo ya Msufini ambapo walimpepea kisha wakammwagia maji ya baridi, akazinduka.
Alipozinduka, aliwaomba marafiki zake wampeleke tena msibani ambapo alipofika aliomba kuletewa mwanaye mdogo, Asantesanaa, akambeba na kukaa naye msibani hapo.CHANZO CHA KIFO
Akizungumza na mwandishi wetu, mama mzazi wa marehemu, Hamida Rajab Sulu, alisema kuwa mwanaye alikuwa akisumbuliwa na ugonjwa wa malaria kali kwa takriban siku tatu, ndipo Jumatano iliyopita asubuhi walipompeleka katika Hospitali ya St. Mary mjini hapa.
Alisema kuwa alipofikishwa hospitalini hapa alilazwa na kuanzishiwa dozi ya malaria lakini baadaye hali ilizidi kuwa mbaya wakalazimika kumuhamishia kwenye Hospitali ya Manispaa ya Morogoro.
“Walimlaza pale kwa saa kadhaa, walipoona hali inazidi kuwa mbaya, walitushauri tumuhamishie kwenye Hospitali ya Manispaa Morogoro.“Tulipofika pale walimuanzishia dripu ya kutibu malaria, kabla hata haijaisha, mgonjwa alianza kutikisa miguu, hapohapo akafariki dunia. Ilikuwa muda wa saa 5:00 usiku,” alisema mama huyo.WASANII WATINGA MSIBANI
Msiba huo umeacha historia ya aina yake kwani kesho yake asubuhi (Alhamisi), wasanii wengi walifika msibani hapo kwa ajili ya kuomboleza hali ambayo iliwafanya baadhi ya watu kushangaa wasanii badala ya kuomboleza.Miongoni mwa wasanii ambao walifika mapema msibani hapo ni pamoja na Rais wa Shirikisho la Filamu Nchini, Simon Mwakifwamba na Joseph Haule ‘Profesa Jay’.
AFANDE ANENA
Akizungumza kwa uchungu makaburini hapo, Afande Sele alisema kifo cha mkewe ni pigo kubwa maishani mwake kwani ndiye aliyekuwa faraja ya pekee kwa wanaye, Tunda na Asantesanaa.
“Hili ni pigo kubwa maishani mwangu, mama Tunda alikuwa ndiye kila kitu kwa wanangu, inaniuma sana,” alisema Afande akitokwa machozi.AZIKWA
Baada ya umati kujikusanya msibani hapo, taratibu za mazishi zilifanyika siku hiyohiyo na wakaelekea kuzika kwenye Makaburi ya Kola mjini hapa.
TUJIKUMBUSHE
Kabla Afande Sele na mama Tunda hawajatengana mapema mwaka huu, waliishi kama mume na mke kwa zaidi ya miaka kumi na kufanikiwa kupata watoto wawili, Tunda na Asantesanaa.