Mtu anaposema tatizo la kutopata ujauzito, ana maana mume na mke walio katika uhusiano wa kutafuta mtoto ndani ya mwaka mmoja, lakini wameshindwa.
Inaweza ikawa zaidi ya mwaka mmoja lakini wastani wa kiwango cha chini ni mwaka mmoja.
Ni tatizo kubwa katika jamii kwani kila mmoja anataka afikie malengo ya kuwa na familia.
Mwanamke na mwanamume wote wanahusika katika tatizo hili japo mara nyingi huonekana ni la mwanamke. Kutoshika mimba kwa muda mrefu ni ugumba ua infertility kwa kitaalamu. Mwanamke au mwanaume anaweza kuwa mgumba.
Ugumba umegawanyika katika maeneo makuu mawili. Kwanza ni ‘primary infertility’ ambapo mwanamke hana historia ya kuwa na mimba wala mwanaume hana historia ya kumpa mwanamke mimba.
Ugumba wa aina ya pili ni ‘secondary infertility’ ambapo mwanamke anayo historia ya kuwahi kupata ujauzito, haijalishi kama alizaaa au mimba ilitoka na mwanamume anayo historia ya kumpa mwanamke mimba na pia haijalishi kama mtoto alizaliwa au mimba ilitoka.
Tatizo la mwanamume kutoweza kumpa mwanamke mimba linaweza kusababishwa na kukosa nguvu za kiume hivyo kushindwa kufanya tendo la ndoa.
Hali hii ya kukosa nguvu inaweza kusababishwa na matatizo mbalimbali kwani yenyewe si ugonjwa.
Kwa hiyo kitu cha msingi siyo kuongeza nguvu bali ni kufanya uchunguzi kuona tatizo ni nini na kulipatia ufumbuzi.
Tatizo lingine kwa mwanamume ni kutotoa mbegu za kiume za kutosha ua kutoa mbegu zisizo na ubora.
Hii ni baada ya kupima kipimo cha mbegu za kiume. Mbegu zinaweza zisizalishwe ua zikazalishwa pasipo na ubora unaostahili kurutubisha yai la mwanamke.
Matatizo mbalimbali yanaweza kuathiri uzalishaji wa mbegu za kiume kama uvutaji wa sigara, unywaji wa pombe kali, maumivu ya korodani na utumiaji wa dawa za kulevya kama mirungi na bangi.
Mazingira ya joto katika korodani pia huathiri uzalishaji wa mbegu. Kutofahamu mzunguko wa hedhi wa mwanamke na kipindi gani mwanaume anaweza kumpa mimba ni changamoto nyingine kwa upande wa mwanaume.
|
0 Comments