Na Anna Nkinda - Washington

Imeelezwa kwamba kutokuwa na uelewa wa kutosha kuhusu ugonjwa wa saratani ya mlango wa kizazi, upungufu wa upatikanaji wa huduma za afya, na vitendea kazi, utungaji wa sera zisizo rafiki, pamoja na ukosefu wa takwimu za magonjwa ni moja ya sababu zinazosababisha wanawake wengi kupoteza maisha kutokana na ugonjwa huo.

Hayo yamesemwa jana na Mke wa Rais Mama Salma Kikwete wakati akitoa neno la shukrani kwa niaba ya wake wa marais wa Afrika waliohudhuria  hafla fupi ya chakula cha mchana  kilichoandaliwa na  kituo cha Marais wa Afrika (African Presidential Centre) cha chuo kikuu cha  Boston iliyofanyika  mjini Washington.

Mama Kikwete ambaye ni Mwenyekiti wa Taasisi ya Wanawake na Maendeleo (WAMA) alisema kwa kiasi kikubwa kuna mahusiano kati ya ugonjwa wa Ukimwi na Saratani ya mlango wa kizazi ambao kama mgonjwa atapata matibabu mapema atapona lakini kutokana na uelewa mdogo baadhi ya wanawake wanapoteza maisha.

“Kutokana na utaalamu uliopo sasa ugonjwa wa Saratani ya mlango wa kizazi unazuilika na kutibika lakini bado kuna uelewa mdogo katika jamii kuhusu uhusiano uliopo kati ya ugonjwa huu na ule wa Ukimwi;  kama zitapatikana fedha za kutosha asasi zisizo za kiserikali ambao ni wawezeshashi wataweza kutoa elimu kwa jamii kuhusiana na magonjwa haya”, alisema Mama Kikwete.