Maafisa wa usalama nchini Kenya walinasa meli kwa jina Amin Darya mwezi uliopita
Serikali ya Kenya imeharibu shehena ya mihadarati aina ya Heroine iliyokuwa imenaswa katika bahari hindi huko Mombasa mwezi mmoja uliopita.
Hii ni baada ya Rais Uhuru Kenyatta kutangaza hapo jana kuwa shehena hiyo itaharibiwa na kuzamishwa baharini na meli iliyokuwa imeibeba.Uharibifu huo wa kilo 370 za heroine ya gharama za ya zidi ya dola milioni 16 za Marekani ulifanyika mwendo wa saa kumi saa za Afrika Mashariki umbali wa maili kumi na nne baharini kutoka katika bandari ya Mombasa.
Maafisa wa jeshi la wanamaji walilipua shehena hiyo na kukasikika mlipuko mkubwa baharini kisha meli hiyo ya kigeni aina ya MV Al Noor ikazamishwa.
Walioshuhudia uharibifu huo walijumuisha maafisa wakuu wa polisi nchini Kenya, wale wa kitengo cha kukabiliana na mihadarati, wakuu wa idara za ujasusi wa mataifa kumi na tatu waliokuwa Mombasa kuhudhuria mkutano wa usalama na jeshi la wanamaji.
Awali mahakama kuu ya Mombasa ilikataa kutoa agizo la kuharibu meli iliyokuwa imebeba shehena hiyo.
Jaji aliyeisikia kesi hiyo iliyokuwa imewasilishwa na afisi ya mkurugenzi wa mashtaka ya umma alisema kuwa hakutaka kuonekana kukinzana na mahakama ya chini ambayo ilikuwa imeelekeza tu shehena hiyo ya heroine iharibiwe.Akitoa onyo kali kuhusu matumizi ya dawa za Kulevya rais Uhuru Kenyatta alisema kuwa hatakubali Kenya kuwa sehemu ya kusafirisha dawa za kulevya kutoka mataifa mengine.
Si mara ya kwanza shehena ya dawa za kulevya kunaswa Mombasa na hatua hii inaonekana ni moja ya jitihada za kupambana na matumizi ya dawa hizo.
Mji wa Mombasa na maeneo jirani ni baadhi ya sehemu ambazo zimeathiriwa pakubwa na matumizi ya dawa za kulevya hususan kwa vijana ambao wamekabiliwa na uraibu wa dawa hizo na kupata madhara ya kiafya.
|
0 Comments