Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Maalim Seif Sharif Hamad akizungumza na waandishi wa gazeti la Mwananchi walioongozwa na Mhariri Mtendaji, Frank Sanga (wa tatu kulia) walipomfanyia mahojiano maalumu kwenye Hoteli ya Serena, jijini Dar es Salaam, hivi karibuni. Picha na Edwin Mjwahuzi
Dar es Salaam. Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Maalim Seif Sharif Hamad amesema kwa mfumo wa muungano uliopo, ni vyema kila upande ukawa unatoa rais kila baada ya miaka 10.
Amesema haiwezekani ziwepo nchi mbili zilizoungana halafu kila akichaguliwa rais awe anatokea upande mmoja tu wa muungano, huku upande mwingine ukiambulia kutoa makamu wa rais.
Mbali na hilo, Maalim Seif pia ametaja sifa tano za rais ajaye huku akisisitiza kuwa kigezo si umri, bali uwezo wake wa kufanya kazi.
Akizungumza katika mahojiano maalumu na gazeti hili Dar es Salaam, Maalim Seif alisema: “Kama ni muungano wa nchi mbili lazima kuwe na mfumo ambao tutajua kwamba kipindi hiki rais ametokea Zanzibar, basi kipindi kingine rais atatoka Bara.”
Tangu Tanganyika na Zanzibar zilipoungana na kuzaliwa Tanzania mwaka 1964, Rais wa Awamu ya Pili wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Ali Hassan Mwinyi ndiye pekee ambaye alitokea Zanzibar. Aliongoza kati ya mwaka 1985-1995.
Akizungumzia Serikali ya Umoja wa Kitaifa kama inaweza kutumika Tanzania Bara, kwa umakini Maalim Seif alisema, “Hilo ndilo suluhisho kutokana na mivutano iliyopo Tanzania Bara. Serikali hii inaunganisha vipaji vya watu ambao wanafanya kazi kwa pamoja.”
Huku akiwa makini na kuonyesha msisitizo wa ishara za mikono, Maalim Seif alisema: “Kwanza rais awe na uwezo wa kuunganisha wananchi kwa sababu ni wa Watanzania wote, kuanzia waliompigia kura na ambao hawakumpigia kura. Asiwe na upendeleo.”
Alisema mtu akishakuwa rais lazima aweke masilahi ya chama chake pembeni na awatumikie wananchi wote.
“Pili, rais anatakiwa kuwa karibu na wananchi kwa sababu sifa za kiongozi mzuri ni kujua hali halisi ya wale unaowaongoza, huwezi kujua hali halisi maisha ya wananchi kama hauko karibu nao,” alisema.
Akitaja sifa ya tatu huku akicheka, Maalim Seif alisema rais ni lazima awe na uamuzi na kuhakikisha kuwa anawabana watu aliowateua.
“Simaanishi rais awe dikteta. Rais unaweza kuwa na baraza lako la mawaziri lakini lazima uwe na malengo yako. Mawaziri wako unawaeleza wazi kwamba katika sekta fulani unataka jambo fulani lifanikiwe, jambo hilo linapendekezwa na kujadiliwa katika kikao cha mawaziri na hatimaye kupitishwa.”Alisema rais ni lazima ajue kuwa jambo fulani lina manufaa au halina manufaa na akichukua uamuzi hatakiwi kuyumba, bali kuusimamia mpaka mwisho.
“Nne, rais anatakiwa kuwa na msimamo na akubali kushaurika. Licha ya kuwa Katiba inaeleza kuwa rais ni mtu mwenye uamuzi wa mwisho lakini ni lazima awe mtu anayekubali kushaurika,” alisema.
Akitaja sifa ya tano, Maalim Seif alisema urais ni taasisi, hivyo rais ni lazima akubali kuisimamia taasisi hiyo... “Rais anatakiwa kutambua kuwa kuna Bunge, Mahakama na Serikali na kila mhimili unatakiwa kufanya kazi bila kuingiliwa. Ukiwa na taasisi imara hata kama utakuwa na rais asiye na uwezo mambo yatakwenda tu.”
Maalim Seif alisema nchi kama Marekani kila mtu anaweza kuwa rais na mambo yakaenda vizuri kutokana na kuwa na taasisi imara.
“Unajua idadi kubwa ya Watanzania ni vijana na pia lazima tujue kuwa vijana wa sasa ni tofauti na ‘vijana’ sisi. Tunahitaji mtu mzoefu. Tusitazame ujana au uzee. Inatakiwa aangaliwe mtu mwenye uwezo wa kuongoza watu. Tunataka rais akiwa kijana asipinge mawazo ya wazee na akiwa mzee lazima ajue matatizo ya sasa ya vijana.”
Huku akitolea mfano wa China, Maalim Seif alisema nchi hiyo licha ya kurekebisha masuala mengi ya uongozi mpaka sasa, Rais na Waziri Mkuu wake ni lazima wawe wa umri zaidi ya miaka 50.
“Unajua wakati mwingine vijana wanakuwa na jazba. Ukiwa rais hautakiwi kutawaliwa na jazba na unatakiwa kuwa na busara, hekima na utaalamu,” alisema.
Katika hatua nyingine, Maalim Seif ameeleza namna viongozi wa Serikali ya Umoja ya Kitaifa Zanzibar, walivyojitahidi kuunusuru mchakato wa Katiba Mpya, huku akisisitiza kuwa sasa umefikia pabaya na ni busara tu ndizo zinazoweza kuunusuru.
Alisema aliwahi kumkatalia Mwenyekiti wa Bunge Maalumu la Katiba, Samuel Sitta alipomfuata kutaka ushauri wake ili kunusuru mchakato huo kwa kuwa taratibu na kanuni za Bunge Maalumu zimevunjwa makusudi.
Alisema alimtaka Sitta kuheshimu maoni ya wajumbe wa Ukawa wanaotokana na vyama vya Chadema, CUF na NCCR-Mageuzi ambao walisusia vikao vya Bunge la Katiba, wakishinikiza ijadiliwe Rasimu ya Katiba iliyotolewa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba.“Mwenyekiti (Sitta) alinifuata na kuomba busara zangu katika jambo hili lakini nikamwambia kama busara hazikutumika ni vigumu kuzipata tena busara hizo.
Lakini maoni yangu yakawa ni yaleyale ya kukubaliana na Ukawa ili kuona jinsi ya kupokea mawazo yao kuliko kulazimisha kuendelea na mchakato eti kwa sababu Ukawa ni wachache.”
Maalim Seif anaamini kuwa kuandika Katiba ni jambo la maridhiano hivyo hata watu wachache nao wana haki ya msingi katika suala hilo na wanawawakilisha wengi.
“Hiyo ilikuwa hatua ya kwanza iliyofanyika. Hatua ya pili ni sisi viongozi wa Zanzibar, mimi, Dk Shein (Ali Mohamed, Rais wa Zanzibar) na Balozi Seif Ali Iddi (Makamu wa Pili wa Rais Zanzibar), tulikaa kujadili jinsi ya kusaidia jambo hili lakini hatimaye likaibuka suala la serikali mbili au tatu na hatukupata mwafaka,” alisema.
Kuhusu nafasi ya Rais Jakaya Kikwete, huku akicheka, Maalim Seif alisema yupo tayari kukutana naye kama akiombwa wazungumze kuhusu mchakato wa Katiba Mpya.
Alipoulizwa kwa nini yeye asimtafute, alijibu: “Sasa nikianza mimi kumtafuta Rais Kikwete wakati tayari nimeanza kuzungumza na wenzangu, Dk Shein na Balozi Seif, nitaonekana kama ninatapatapa.”
Hata hivyo, Maalim Seif alisema Rais Kikwete ndiye mtu pekee anayeweza kunusuru mchakato wa Katiba kwa sababu awali aliaminika na watu wote kwa tabia yake ya kukutana na makundi mbalimbali kila yalipokuwa yanatofautiana.
“Kilichotokea sasa ni Rais kukubali kushawishiwa na chama chake. Mwanzo kanuni zilitungwa kwamba rais atalizindua Bunge halafu atafuata Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba (Jaji Warioba) kuwasilisha Rasimu. Wao wakabadilisha na kulazimisha aanze Warioba na kutaka kumpa saa moja tu ya kuzungumza,” alisema.
Alihoji: “Mtu aliyetembea Tanzania nzima kukusanya maoni ya wananchi unataka kumpa saa moja kuwasilisha rasimu, halafu anakuja Wako (Mwanasheria Mkuu mstaafu wa Kenya, Amos) unampa siku nzima.”
Alisema suala hilo liliibua mvutano mkali na kusababisha wapinzani kutishia kugoma na baadaye suluhu ikapatikana kwamba Jaji Warioba apewe saa nne kuwasilisha Rasimu, lakini awe wa kwanza na Rais Kikwete afuate.
“Rais haikuwa jukumu lake kupinga alichokisema Warioba. Nakumbuka alivyozungumza na Baraza la Vyama vya Siasa alinifurahisha kwa sababu alizungumza kama Rais wa nchi na hakuegemea upande wowote na alisema wazi kwamba tusidhani wingi ndiyo utapitisha Katiba na kwamba Katiba ni maridhiano,” alisema.
Huku akicheka alisema: “Sijui ni nini kilitokea. Rais alifungua Bunge na kuchukua moja kwa moja msimamo wa chama chake na kuanzia hapo ndipo mambo yalipoanza kuharibika. Bado Rais anayo opportunity (fursa) kwa sababu Ukawa wanachotaka ni kuhakikishiwa kuwa wanakwenda katika Bunge kujadili Rasimu iliyowasilishwa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba.”Alipoulizwa kama Katiba Mpya itaweza kupatikana kama Ukawa wataendelea kususia vikao vya Bunge hilo, alisema jambo hilo halitawezekana kwa sababu haitapatikana theluthi mbili ya wajumbe kutoka Zanzibar kwa ajili ya kupiga kura ya kufanya uamuzi.
“Ndiyo maana nikasema tunatakiwa kuwa na rais wa Watanzania wote akatazame hoja kama za Ukawa ili kuona kama zina msingi wowote maana kama hoja zisingekuwa za msingi, Ukawa wasingetoka,” alisema.
Alisema kuwa rais ni mtu mzima, si lazima awaombe radhi Watanzania, bali anaweza kutoa lugha nzuri na watu wakamwelewa kuwa aliteleza katika hotuba yake ya kulifungua Bunge la Katiba.
Kuhusu Ukawa kuachiana majimbo katika Uchaguzi Mkuu mwaka 2015 alisema, uamuzi wa mwisho bado haujachukuliwa lakini maoni yaliyopo ni Ukawa kuendelea hata baada ya mchakato wa Katiba.
“Kwanza tunaangalia jinsi tutakavyoweza kushirikiana katika Uchaguzi Mkuu unaokuja, lakini hili nataka liwekewe mikakati yake kwa sababu huko nyuma tulishajaribu lakini tukaachana njiani, sasa hatutaki hayo yatokee. Tuliachana njiani kwa sababu hatukujiandaa vizuri.”
|
0 Comments