Doroth Myunga akionyesha bidhaa zake katika maonyesho ya Nanenane yaliyofanyika katika Viwanja vya John Mwakangale jijini Mbeya hivi karibuni. Picha na Hawa Mathias      
Mbeya. Ni katika Viwanja vya Maonyesho ya Nanenane vya John Mwakangale jijini Mbeya ndipo mjane Doroth Myunga anaeleza machungu ya maisha aliyokumbana baada ya kufiwa na mume wake mwaka 2005.
Anasema kuwa ugumu wa maisha aliokumbana nao ulimfanya apate akili ya kujikita katika kilimo kwa mtaji wa Sh1.3 milioni, baada ya kuuza ng’ombe mmoja aliyeachiwa kama urithi na marehemu mumewe.
Doroth alihitimu elimu ya msingi katika Shule ya Msingi Igula, Tarafa ya Isimani.
Kata ya Kihorogoto mkoani Iringa Mwaka 1989, lakini hakupata fursa ya kuendelea na elimu ya sekondari kutokana na kukosa msaada wa kuendelezwa kwani wazazi wake hawakuwa na uwezo.
Anaeleza kuwa mbali na kujikita katika kilimo, amekuwa akijihusisha pia na ujasiriamali wa kutengeneza urembo wa mapambo ya nyumbani ofisini kwa kutumia shanga ili kujipatia fedha.
Anasema kuwa bidhaa hizo za urembo amekuwa akiziuza kwa kati ya Sh50,000 hadi Sh150,000 kulingana na mahitaji ya wateja wake.
Doroth anasema kuwa kutokana na shughuli za ujasiriamali, ameweza kujipatia Sh,300,000 kwa siku, fedha ambazo zinamsaidia kujikimu na hali ya maisha licha ya kujikita katika kilimo pia.
Anasema kuwa ujane alionao haukumfanya kukata tamaa ya maisha, bali aliendelea kupambana na kujikita zaidi katika kilimo na kuhamasisha wanawake wengine kijijini kuanzisha kikundi na kuwa na shamba la mfano, ambalo kwa kiasi kikubwa lilimekuwa mkombozi.
“Tumeweza kulima alizeti na kupata magunia 18 ambayo tuliuza na kupata zaidi ya Sh2 milioni za kikundi,”anasema.
Anabainisha kuwa walianza kukopeshana fedha hizo kwa kila mwanachama kupata Sh200,000 hali iliyompatia mwanga kuwekeza zaidi katika kilimo na kutokana tamaa.
Anaeleza kuwa kutokana na mtaji huo kwa msimu huu wa kilimo amefanikiwa kupata magunia 40 ya alizeti ambayo anatarajia kuuza ili aweze kuboresha zaidi maisha yake.
Doroth anasema kuwa kilimo kimempa mafanikio makubwa na kwamba mpaka sasa ameweza kumiliki trekta lenye thamani ya Sh39 milioni, hali iliyomwezesha kuachana na kilimo cha jembe la mkono na kulima kisasa hivyo kujikuta akipata mazao mengi zaidi.Mwanamke huyo anasema kuwa matarajio yake ni kujenga nyumba ya kisasa kujikita katika usindikaji wa zao la alizeti kwa kuchuja mafuta na kutafuta zabuni ya kusambaza mashudu kwa wananchi wanaojihusisha na ufugaji.
Doroth anabainisha kuwa wameweza kupata mikopo mbalimbali katika kikundi chao kupitia katika Halmashauri ya Mji wa Iringa kwa lengo la kuboresha kilimo cha mazao ya chakula na biashara hasa kwa wajane walio vijijini.
Wito
Doroth anatoa wito kwa wanawake kuwa wasichukulie hali hiyo kuwa ni sababu ya kubweteka na kukimbilia kuolewa au kulalamika, badala yake wajitume katika shughuli mbalimbali za kijamii hasa kuanzisha miradi midogo ya ujasiriamali ili kujiopatia fedha na kutunza familia zao wakiachana na dhana ya kurithiwa au kuolewa tena.
“Ujane isiwe changamoto kwa wakinanamama bali ni kupambana na maisha kwa kujishughulisha na kilimo na kuanzisha miradi ya ujasiriamali ili kujikwamua kiuchumi,”anasema.
Doroth anasema kuwa wakati umefika kwa wajane kuwa katika vikundi ili Serikali iweze kuwatambua na kuwapatia mikopo yenye riba nafuu ili kuweza kujinasua katika hali duni ya masha na utegemezi katika familia.
Anaweka wazi kuwa binafsi aliwahi kushiriki Shindano la Mama Shujaa wa Chakula mwaka 2012, ingawa hakufanikiwa kupata nafasi, lakini hakati tamaa akiamini ipo siku atafanikiwa kwani yeye ni mkulima hodari.
Changamoto
Anasema kuwa wakulima wa vijijini wamekuwa na changamoto ya ukosefu wa miundombinu mizuri ya barabara, maji na nishati ya umeme hali inayosababisha kutofikia ndoto zao za usindikaji wa mazao wanayozalisha.
Anaiomba Serikali kuwezesha wakulima wa vijijini kwa kuhakikisha wanafikiwa na wataalamu wa kilimo ili kuboresha kilimo kilicho na tija na kupata soko la ndani na nje ya nchi pamoja na kupata pembejeo za kilimo hususan matrekta madogo.
Doroth anaomba wadau mbalimbali nchini kusaidia kutetea haki za wajane akisema kundi hilo limekuwa na changamoto kubwa ya kuporwa mali wanazoachiwa na waume zao wanapofariki.