Stori: Sifael Paul na mitandao Kufuatia vurugu zilizoibuka ukumbini alfajiri ya Jumapili iliyopita baada ya msanii Nasibu Abdul ‘Diamond Platnumz’ kucheleweshwa kupanda stejini kwenye Ukumbi wa Sindelfingen uliopo Mji wa Stuttgart, Ujerumani, mwanamuziki huyo anadaiwa kupigwa marufuku kutia maguu nchini humo.SHUHUDA WETU Kwa mujibu wa chanzo chetu makini mjini humo, ambacho pia kilikuwepo ukumbini wakati vurugu zilipoibuka, uchunguzi wa awali umeonesha kwamba, gharama ya vitu vilivyoharibiwa inakadiriwa kuwa zaidi ya Euro 128,322 sawa na Sh. milioni 280.“Tukio la vurugu za Diamond limeripotiwa kwenye magazeti tofauti mjini hapa lakini kubwa ni hasira ambayo mashabiki wa Diamond wameionesha waziwazi. “Kwa mfano Gazeti la Stuttgarter la leo (Jumatatu) la mjini hapa limeandika:‘MASHABIKI WANA HASIRA NA DIAMOND’.
Kwenye habari zao waliwahoji watu waliofurika ukumbini hapo. “Wengi walikuwa wakilalamika kwamba walikata tiketi mapema kwa euro 25 (zaidi ya Sh. elfu 55) kwa kichwa. Yaani kuanzia saa 4:00 watu walikuwa tayari wanamsubiri Diamond.
MUDA WAYOYOMA “Kuna muda DJ alitangaza kwamba angepanda stejini kuanzia saa 6:00 usiku hivyo watu wakapunguza hasira. Cha ajabu saa saba ilikatika, nane ikapita, tisa ndipo mtiti ukaanza.“Sasa hebu fikiria mtu umetoa buku 55 yako halafu hadi saa tisa usiku mtu haonekani! Hapo ndipo tatizo lilipoanzia!” yamesomeka hivyo magazeti ya hapa.Ilisemekana kwamba ilipofika saa 10:00 alfajiri ndipo Diamond alipoletwa jukwaani na promota wake, raia wa Nigeria anayejiita Kamabritts.
CHUPA ZARUSHWA Mashabiki walipoona kuwa hawakutendewa haki walianza kurusha chupa na kutaka kumvamia mwanamuziki huyo na promota wake.Ilidaiwa kwamba kilichowakera zaidi mashabiki hao ni vyombo vibovu vilivyofungwa ukumbini humo kitu ambacho kiliwafanya kuvunjavunja viti, meza, jukwaa na vyombo vya muziki kisha kusababisha watu kujeruhiwa na hasara kubwa ya mamilioni ya shilingi.MAJERUHI WAONGEZEKA
Baadhi ya vyombo vya habari mjini humo, juzi (Jumatatu) viliripoti kuongezeka kwa majeruhi wakiwemo MaDJ wawili ambao hali zao bado ni tete hospitalini kwa sasa. Katika vurugu hizo, DJ mwanamke aliyetajwa kwa jina la DJ Flor alizimia hivyo akakimbizwa hospitalini huku mashabiki wakimpa kipigo DJ Drazee.
KAULI YA POLISI Polisi eneo la Sindelfingen, Stuttgart nchini Ujerumani walisema tukio hilo ni la aibu hivyo uchunguzi wa kina unaendelea ambapo promota huyo na Diamond watalazimika kulipa vitu hivyo na kwamba hawatawaruhusu kufanya tena shoo eneo hilo na kwingineko nchini humo.Vyombo vya habari vya Ujerumani viliandika kuwa polisi wamesema walitenga askari 18 wa kutuliza ghasia ambapo walifyatua mabomu ya machozi ili kumuokoa Diamond.Walisema kwamba kitendo cha msanii kuchelewa kufika jukwaani nchini humo ni kitu cha hatari mno kwani mashabiki wanaheshimu muda wao.
PROMOTA ASAKWA Hadi gazeti hili linakwenda mitamboni polisi walikuwa wakimsaka promota huyo, Kamabritts ili wamalizane na Diamond aruhusiwe kuondoka nchini humo na asirudie tena jambo kama hilo.
MCHEZO NYUMA YA PAZIA Duru za kiuchunguzi zinaonesha kwamba, shoo nyingi za wasanii kutoka Afrika zinazofanywa kwenye kumbi mbalimbali katika baadhi ya nchi za Ulaya, hucheleweshwa makusudi ili vinywaji viuzike.Ilidaiwa kwamba, katika tukio hilo baya, kulikuwa na tatizo la kiusimamizi kwani mbali na promota, menejimenti ya Diamond ilipaswa kuwa na ratiba kamili na siyo kumsikiliza promota ambaye anawaza zaidi kuingiza kipato kuliko heshima ya msanii hivyo jamaa huyo kuwa staa wa kwanza kutoka Afrika Mashariki kusababisha vurugu Ulaya.
LAWAMA KWA MENEJA WA UJERUMANI Kuna maelezo kwamba, Diamond huwa ana mameneja wengi kwenye kila nchi anayokwenda hivyo huyo meneja wa Ujerumani alistahili lawama zote kwani alipaswa kujua kinachoendelea ukumbini.
BABU TALE ANASEMAJE? Kuhusu hilo, Risasi Jumatano lilimtafuta meneja wa Diamond ambaye hakusafiri na msanii huyo, Babu Tale na kuulizwa kulikoni yaliyomkuta Diamond Ujerumani ambapo alikuwa na haya ya kusema: “Kweli inasikitisha lakini haukuwa mpango wa Diamond. Ninachojua alikuwa akimsikiliza promota.
Ni changamoto kubwa lakini tunaomba radhi kwa mashabiki wetu wa Ujerumani. Next time wampokee vizuri.“Lakini kwa upande mwingine unajua ni jambo kubwa na niseme tu kuwa ukilitazama tukio hili kibiashara ni kama limemkuza zaidi kujulikana duniani. Umeona ameripotiwa na vyombo vingi vya habari. Mitandao ya kijamii ndiyo usiseme. Yote kwa yote tumejifunza na tunaomba radhi. Tusiangalie tulipoangukia, tuangalie tulipojikwaa.”
|
0 Comments