Mjumbe wa Bunge Maalumu la Katiba, Maria Sarungi akizungumza wakati wa kongamano la kujadili Mchakato wa Mabadiliko ya Katiba lililoandaliwa na Taasisi ya Tanzania Youth Vision Association (TYVA) jijini Dar es Salaam jana.  Picha na Rafael Lubava. 

Dodoma. 
Wakati Rais Jakaya Kikwete akitarajiwa kukutana tena na viongozi wa vyama vya siasa ambavyo ni wanachama wa Kituo cha Demokrasia nchini (TCD), kuna taarifa kwamba huenda Oktoba 4, mwaka huu ikawa siku ya mwisho ya kukutana kwa Bunge Maalumu, linaloendelea na utunzi wa Katiba Mpya mjini Dodoma.
Mkutano wa Rais Kikwete na viongozi hao kutoka vyama vyenye wabunge na kimoja kinachowakilisha vyama visivyokuwa na wawakilishi bungeni, unajadili kwa undani mustakabali wa uchaguzi mkuu ujao, hali inayoashiria kwamba suala la Katiba Mpya siyo tena kipaumbele cha sasa katika siasa za nchi.
Kamati ndogo iliyoundwa na TCD chini ya Mwenyekiti wa NCCR- Mageuzi, James Mbatia itawasilisha mapendekezo ya majawabu ya hoja zilizopendekezwa katika mkutano wa awali uliofanyika Agosti 31, mwaka huu katika Ikulu ya Kilimani, Dodoma na baadaye kuhitimishwa na kikao cha faragha cha viongozi wa vyama hivyo katika Hoteli ya St Gaspar.
Mbali na Mbatia wajumbe wengine ni wale wanaotoka kwenye vyama ambavyo viko kwenye mvutano kuhusu Bunge Maalumu wakiwamo wale wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) kwa upande mmoja na CCM kwa upande mwingine.
Hao ni Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba, Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Willibrod Slaa wakati CCM kinawakilishwa na Katibu Mkuu wake, Abdulrahman Kinana ambao kwa pamoja watawasilisha mapendekezo ya kumaliza mvutano uliopo pamoja na mwafaka kuhusu namna bora ya kuendesha uchaguzi mkuu ujao.
Taarifa ambazo gazeti hili lilizipata zinasema miongoni mwa mambo ambayo yamekuwa yakisukumwa kwa nguvu na Ukawa hata walipokutana na Rais mara ya kwanza ni kusitishwa kwa Bunge Maalumu kwa maelezo kwamba Katiba Mpya siyo tena kipaumbele cha nchi na kwamba fedha zinazotumika zingeelekezwa katika mambo mengine muhimu ya nchi.
Ukawa unaoundwa na vyama vya NCCR- Mageuzi, CUF na Chadema, wajumbe wake katika Bunge Maalumu walisusia vikao vya Bunge hilo tangu Aprili 16, mwaka huu kwa maelezo ya kwamba hawaridhishwi na mambo yanavyoendeshwa na baadaye kuanza kushinikiza kusitishwa kwake.
Hata hivyo, suala la kusitishwa kwa Bunge Maalumu limekuwa gumu kutokana na kutokuwapo kwa mwanya wowote wa kisheria unaomruhusu Rais Kikwete kuchukua hatua hiyo, lakini habari zinasema ‘mlango pekee uliobaki’ ni Oktoba 4, 2014 ambayo ni siku ya mwisho iliyotajwa kwenye tangazo la Serikali.
“Nadhani hata mheshimiwa Rais ameshaombwa asitoe GN (tangazo lingine) ya kuongeza siku za Bunge Maalumu kama wajumbe wa Bunge wanavyotaka, kwa hiyo kama atakubali ni dhahiri kwamba Bunge litakoma tarehe 14 mwezi ujao (Oktoba),” kilisema chanzo chetu kutoka serikalini.
Ikiwa Rais ataamua kutobadili tangazo lake, basi Bunge Maalumu litasitisha shughuli zake, kwani tayari lilishapanga ratiba inayoonyesha kuwa litaendelea hadi mwishoni mwa Oktoba wakati Mwenyekiti wake, Samuel Sitta atakapokabidhi Katiba inayopendekezwa kwa Rais Kikwete.
Tarehe ya mwisho
Licha ya tarehe ya mwisho ya Bunge hilo ambayo ni Oktoba 4, 2014 kutangazwa na Rais Kikwete Julai 28 mwaka huu na kuchapwa kwenye Gazeti la Serikali (GN) namba 254 la Agosti 1, 2014, Bunge Maalumu lilibadili kanuni zake, hatua ambayo ilitaja siku sitini zilizotolewa na Rais kwamba ni za kazi tu.Awali katika azimio lake la Aprili 4, mwaka huu, Bunge Maalumu liliipitisha Jumamosi kuwa moja ya siku zake za kazi kwa kuongeza kipengele cha nne katika Kanuni ya 14. Sehemu ya Kanuni hiyo inasomeka: “Bunge Maalumu kwa siku za Jumamosi litakutana kuanzia saa tatu asubuhi hadi saa saba mchana…..”.
Hata hivyo, Agosti 5, 2014 Bunge hilo lilipitisha azimio lingine ambalo lilirekebisha kanuni hiyo ya 14 (4) na kuifuta Jumamosi katika siku zilizotajwa kuwa za kazi. Sitta aliwaambia wajumbe wa Bunge hilo kwamba Rais Kikwete alikuwa tayari ameridhia kwamba siku 60 alizotoa hazitajumuisha Jumamosi, Jumapili na siku za sikukuu.
Baada ya mabadiliko hayo, Katibu wa Bunge Maalumu, Yahya Khamis Hamad aliandika barua serikalini akitaka ufafanuzi wa kisheria kuhusu suala hilo, lakini hadi sasa barua hiyo haijajibiwa.
Katibu Mkuu Kiongozi, Ombeni Sefue wiki hii aliliambia gazeti hili kwamba Rais Kikwete alikuwa amepokea maombi ya Bunge Maalumu ili arekebishe tangazo lake la awali na kwamba bado yanafanyiwa kazi huku akisisitiza kuwa uamuzi wa Rais lazima utazingatia sheria.
Sefue alitoa kauli hiyo huku akisema Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Jaji Frederick Werema alikuwa sahihi katika tafsiri aliyowahi kuitoa akisema kwamba siku zinazotajwa kwenye gazeti la Serikali kwa ajili ya Bunge Maalumu ni za kikalenda na siyo za kazi kama ilivyotafsiriwa na uongozi wa Bunge hilo.
Mwanasheria katika Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu, Harold Sungusia akizungumzia suala hilo jana alisema kifungu cha 28 cha Sheria ya Mabadiliko ya Katiba ndicho kinachoelekeza jinsi nyongeza ya siku inavyopaswa kufanyika wakati kifungu cha 27 (3) cha sheria hiyo pia kinalipa Bunge Maalumu uwezo wa kutunga kanuni za jinsi ya kuendesha mambo yake.
“Sheria iko wazi na hapa tafsiri sahihi ya siku zilizoongezwa inaweza kutolewa na mahakama kwani Mwanasheria Mkuu wa Serikali hana nafasi katika Bunge hili na hapo ndipo tatizo lilipo kwamba kuna watu wanadhani kwamba hili ni Bunge la kawaida, sivyo hata kidogo,”alisema Sungusia.
Hoja ya kutaka Bunge Maalumu kusitishwa mapema kama ilivyo kwenye tangazo la Serikali inatokana na ukweli kwamba ratiba yake ya sasa inaingiliana na ratiba za vikao vya Bunge la Muungano ambalo limepangwa kuanza Novemba 4, 2014 na Baraza la Wawakilishi ambalo limepangwa kukutana kuanzia Oktoba 22 mwaka huu.
Kwa upande wa Bunge la Muungano, Katibu wake Dk Thomas Kashililah alisema kuna kamati za kisekta zinapaswa kuanza vikao vyake Oktoba 10 kwani kuna miswada mingi ya Serikali inayopaswa kufanyiwa kazi mapema.
Rais na TCD
Mwenyekiti wa TCD, John Cheyo aliliambia gazeti hili mjini Dodoma siku chache zilizopita kwamba mazungumzo baina yao na mkuu huyo wa nchi yanalenga mambo muhimu ya kuwezesha kuwa na mazingira bora ya uchaguzi mkuu wa 2015 na siyo vinginevyo.
“Tuna mambo muhimu na hayo diyo tumekuwa tukizungumza, mambo ya Tume Huru ya Uchaguzi, mambo ya mgombea binafsi, kuhojiwa kwa matokeo ya urais, hayo ndiyo mambo tunayozungumza kuona jinsi gani tutaweza kuwa na mwafaka wa pamoja maana hata kama Katiba Mpya ikipitishwa leo haiwezi kutumika kwenye uchaguzi mkuu,” alisema Cheyo ambaye pia ni Mwenyekiti wa Taifa wa UDP.Baada ya mkutano wa Agosti 31 mwaka huu katika Ikulu ya Kilimani, Dodoma na baadaye katika Hoteli ya St Gaspar pia ya mjini humo, viongozi wote walitoa tamko la pamoja ambalo pamoja na mambo mengine lilitaja kuundwa kwa kamati ndogo ili kuzifanyia kazi hoja kadhaa zilizowasilishwa kwenye kikao hicho.
Habari zilizopatikana jijini Dar es Salaam zinasema kamati hiyo ilifanya vikao vyake jijini Dar es Salaam na leo wajumbe wake watasafiri hadi Dodoma kwa ajili ya mkutano wa awamu ya pili na Rais Kikwete.