Msikiti ambao unasemekana kuunga mkono watu wanaoshiriki mapenzi ya jinsia moja, na ambao pia wanawake wataruhusiwa kuswali ndani,umefungwa.
Afisaa mmoja mjini Cape Town, anasema kuwa msikiti huo umevunja sheria za baraza la jiji kwa kukosa nafasi za kuegesha magari ya waumini.
Msikiti huo, ulifunguliwa rasmi siku ya Ijumaa wiki jana licha ya kukosolewa na waumini wa kiisilamu katika eneo uliko.

Mwanzilishi wa msikiti huo, Taj Hargey, alisema kuwa msikiti huo utasaidia katika kupambana na kuenezwa kwa itikadi kali za kidini.
''Tunafungua msikiti huu kwa watu walio na muonekano chanya kwa baadhi ya mambo wala sio wenye muonekano finyu,'' alisema bwana Hergey kabla ya ufunguzi wa masikiti huo.
Kadhalika bwana Hargey alikana kwenda kinyume na mafunzo ya dini ya kiisilamu.
Maafisa wa baraza la jiji wamekanusha madai kuwa kufungwa kwa msikiti huo ni kwa nia mbaya."swala hili linazua sana hisia, baadhi ya maafisa wa baraza la jiji, ambao ni waisilamu wangeteka kuunga mkono kufungwa kwa msikiti huo, lakini wasio waisilamu wangependa kuuona ukiwa wazi, lakini cha muhimu hapa ni kwamba, tungetaka kuona sheria ikifuatwa, '' alisema afisa mmoja wa baraza la jiji.
Inaarifiwa kuwa bwana Hargey hakuomba idhini ya kuruhusu jengo lililokuwa likitumiwa kama sehemu ya kuweka vitu kubadilishwa na kuwa msikiti.
Kuambatana na masharti ya baraza la jiji, kila sehemu ya maombi inapaswa kuwa na sehemu ya kuegeshea magari ya waumini lakini msikiti huo hauna sehemu hiyo.
Shughuli ya kuwasilisha maombo ya kuwezesha kuwepo sehemu ya kuegeshea magari huenda ikachukua hadi miezi sita.
Bwana Hargey aliambia BBC kwamba anaamini kuwa kila kitu kiko shwari.
Wanawake wataruhusiwa kuswali pamoja na wanaume na hata kuongoza maombi.