Stori: Makongoro Oging’ na Haruni Sanchawa
MH! Hatimaye yule mwanaume aliyedaiwa kufumaniwa na mke wa mtu na hatimaye kufanyiwa usodoma na  watu sita, akiwemo mume wa mwanamke huyo amefungukia mchezo mzima.Hivi karibuni mwanaume huyo (jina tunalo) ambaye ni mume wa wake wawili na mkazi wa Yombo Kiwalani, Wilaya ya Ilala jijini Dar mwenye umri wa miaka 34 alikutwa  na mkasa huo kwenye nyumba ya kulala wageni iitwayo Yombo Executive inayomilikiwa na Athuman Maembe (pichani).
Mara baada ya picha za tukio hilo kuenea kwenye mitandao ya kijamii na watu kushangaa, gazeti hili lilituma timu yake ya habari za uchunguzi ili kupata ukweli wa tukio hilo.Uwazi lilifanikiwa kumpata mwanamume huyo ambaye ni mfanyabiashara, pia alijitambulisha kuwa yeye ni mwelimishaji rika wa magonjwa ya ngono, afya ya uzazi, madawa ya kulevya na unyanyasaji wa kijinsia.
Alianza kwa kusema: “Ni kweli mimi ndiye niliyetendewa ukatili ule. Natamani kujiua kwani mambo yale nayasikia tu usiombe yakukute.
“Nimefedheheka sana, sina mahala pa kuficha aibu hii kubwa. Kila nikikumbuka kuwa nina wake wawili na watoto, wazazi, marafiki na ndugu, bora hata wangeniua kuliko kuniacha nazidi kudhalilika hivi.
“Siku ya tukio ilikuwa Jumamosi ya Agosti 23, mwaka huu. Kuna mwanamke mmoja anaitwa mama Lilly alinipigia simu. Kwanza alikuwa akinipigia simu mara kwa mara wiki moja kabla ya tukio akinieleza kwamba ana shida na mimi, alisema mume wake amekuwa akimnyanyasa kijinsia.
“Siku hiyo, saa tatu asubuhi mama Lilly alinipigia simu huku analia, akasema  kwamba mumewe kampiga na kumfukuza nyumbani hivyo anaomba kuonana na mimi kwa ajili ya ushauri ila alitaka tukutane naye maeneo ya Mtongani, Mbagala au Tandika.“Nilikataa, nikamwambia aje kwenye Ukumbi wa Maembe ninakotoaga mafunzo mbalimbali kwa vijana. Ukumbi huo upo karibu na nyumba hiyo ya kulala wageni kulikotokea tukio.

“Huyu mwanamke namfahamu kwani kipindi cha nyuma alikuwa na stationary karibu na maeneo haya, nilikuwa nikimtengenezea kompyuta lakini miaka miwili iliyopita alihama na sikujua alipo hadi hivi karibuni aliponipigia simu.
“Basi, nilipomwambia aje yeye maeneo haya, aliamua kunifuata. Alifika saa saba mchana huku akibubujikwa machozi, nilimsikiliza kwa makini matatizo yake mwishowe aliniomba nimkopeshe shilingi laki moja ili aende kwao, nilimjibu kwa pale sikuwa nazo labda mpaka Jumatatu.
“Akasema kama ni hivyo basi nimsaidie sehemu ya kulala ili kesho yake aondoke kwenda kwa dada yake. Nilimuonea huruma, nilimchukulia chumba, nikamwambia kama kutakuwa na tatizo anipigie simu. Wakati najiandaa kutoka chumbani aliendelea kuongea maneno mengi sana ya kunifanya niendelee kuwepo.
“Wakati huo alikuwa akituma ujumbe wa simu sehemu nisiyoijua. Sasa nilipoagana naye, ile natoka tu, mlangoni niliona wanaume sita wakanirudisha chumbani na kufunga mlango.“Wakaniambia niwape namba yangu ya akaunti ya benki na password ya simu yangu kwani walijua kwamba tayari nimetumiwa fedha kutoka nje ya nchi kutoka kwa wafadhili.“Niliwaambia sina akaunti, wakanipiga sana, ikabidi niwaongopee kwamba nyumbani nina shilingi laki tano, wakaniambia niwaelekeze nyumbani, nikafanya hivyo. Wawili kati yao waliondoka na pikipiki hadi kwangu kuchukua fedha, wengine wakawa wamenizuia chumbani na kunitishia nikipiga kelele ndiyo mwisho wa maisha yangu.
“Wale walipofika kwangu walimwambia mke wangu awape laki tano na walimtaka aongee na mimi kwa simu huku nikiwa chini ya ulinzi. Mke wangu aliwaambia hana fedha hizo ana laki moja tu, nilimwambia awape.“Waliporudi  na shilingi laki moja walisema nimewadanganya, wakaniadhibu na kunivua  nguo, wakanilawiti kwa zamu na kunilazimisha kuwafanyia mambo ambayo ni tabu hata kuyasema huku wakinipiga picha.
“Baada ya kumaliza walichukuwa laptop, nguo na simu wakaondoka huku wakiniambia ifikika Jumatatu, yaani siku moja baada ya tukio niwape shilingi milioni moja la sivyo wanaweka picha zangu mtandaoni.
“Hata hivyo, baada ya kukosa hizo fedha waliziweka picha mtandaoni, ikawa napigiwa simu na watu mbalimbali walioziona.“Waliponiacha pale chumbani nikiwa  sina nguvu, nilichukuwa shuka nilijikokota mpaka kwa meneja wa gesti na kumweleza. Alinipa nguo yake ili niweze kwenda Kituo Kidogo cha Polisi cha Minazi Mirefu kutoa taarifa na baadaye  Buguruni na kufungua kesi yenye jalada namba BUG/RB/8520/2014 Kujipatia Fedha kwa Njia ya Udanganyifu lakini baadaye ikaongezwa shitaka lingine la kulawiti.
“Kinachonishangaza ni kwamba iweje wanaume hao sita waingie na kutoka bila wenye gesti kuwabaini?” alihoji mwanaume huyo.
Naye mmiliki wa nyumba hiyo ya wageni alikiri kupokea taarifa ya kutokea kwa tukio hilo na kudai kwamba ni la aibu na kusema suala hilo linashughulikiwa na jeshi la polisi.
Kamanda wa Mkoa wa Kipolisi Ilala, SACP, Mary Nzuki alipohojiwa na mmoja wa waandishi wa habari hii ofisini kwake mwishoni mwa wiki iliyopita alikiri kutokea kwa tukio hilo na kusema tayari watuhumiwa wanne wanashikiliwa Kamanda Nzuki aliwataja wanaoshikiliwa kuwa ni Erick Kasila, Sanifa Sadik, Shela Sadik na Juma Richard.