Rais wa Marekani Barack Obama ametumia hotuba yake katika kikao cha baraza la Umoja wa Mataifa kuomba ushirikiano wa mataifa mengine katika vita dhidi ya kile alichokitaja kama mtandao wa chuki, mauaji na uhasama.
Matamshi ya Obama yalilenga kundi la wapiganaji wa kiisilamu la Islamic State nchini Syria.
Rais Obama, amesema kuwa Marekani itatumia nguvu kwa ushirikiano na washirika wake na kuwafunza pamoja na kuwapa silaha wanajeshi wanaopambana na I-S , wakati ufadhili wa kundi hilo ukiangamizwa.
Rais Obama atakuwa mwenyekiti wa mkutano wa baraza la usalama la Umoja wa Mataifa utakaofanyika baadaye mwaka 2000.

Alisema kuwa watafikia azimio ambalo litaeleza jukulu la kila nchi katika kupambana na uenezwaji wa itikadi kali ambao unaambatana na ghasia.
Awali, katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon, alizungumzia unyama unaotendwa na kundi la Islamic State na alichokiita mauaji yanayoendelezwa na wapiganaji wa Boko Haram.Wakati huohuo, ndege za kivita za Marekani zimefanya mashambulizi ya angani dhidi ya wapiganaji wa Islamic State nchini Iraq na Syria, na kuharibu magari na maeneo yenye silaha.
Taarifa hii ni kwa mujibu wa jeshi la Marekani.
Magari manane ya IS yaliharibiwa karibu na eneo la Abu Kamal upande wa mpaka wa Syria na Iraq pamoja na maeneo mengine mawili ya Deir al-Zour Mashariki mwa Syria.
Nchini Iraq, mashambulizi yalifanywa dhidi ya IS Magharibi mwa Baghadad na Kusini Mashariki mwa Irbil karibu na eneo la Kikurdi.