Polisi nchini Nigeria wamedaiwa kuwatesa wanaume na wanawake pamoja na watoto. Taarifa hii ni kwa mujibu wa shirika la kutetea haki za binadamu la Amnesty International.
Shirika hilo limechapisha ripoti yake ambayo inadai kwa watu huzuiliwa kinyume na sheria Kaskazini Mashariki mwa Nigeria ambako jeshi la serikali linapambana na wanamgambo wa Boko Haram.
Serikali ingali kujibu tuhuma hizo.
Shirika hilo linasema kuwa jeshi la Nigeria pamoja na polisi hutumia mbinu tofauti kuwatesa watu ikiwemo kuwapiga, kuwadunga misumari na kuwang'oa meno, ubakaji na dhuluma nyinginezo za kingono.
Kwa mujibu wa ripoti hiyo wanajeshi huwatesa watu zaidi katika eneo la Mashariki ambako vita dhidi ya Boko Haram ni vikali zaidi.
Shirika hilo linasema kuwa kati ya watu efu tano na elfu 10 wamekamatwa tangu mwaka 2009 na kunyongwa katika kambi za wafungwa.
Ripoti hiyo yenye mada, "Welcome to hell fire", inatoa taswira mbaya sana kuhusu haki za binadamu kote nchini Nigeria, na inasema kuwa vituo vingi vya polisi vina afisaa wa polisi anayesimamia mateso na kutaka watu kulipa hongo ili kukwepa mateso hayo.
Licha ya kuharamisha mateso, shirika la Amnesty linasema kuwa wanasiasa nchini humo bado hawajapitisha sheria inayowachukulia hatua wale wanaohusika na mateso dhidi ya raia wasio na hatia.
|
0 Comments